Wafungwa 129 wauawa wakijaribu kutoroka jela DRC
Kwa akali watu 129 wamethibitishwa kuawa na wengine 59 kujeruhiwa wakati wa jaribio la kutoroka jela katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa DRC, Shabani Lukoo amesema leo Jumanne katika taarifa aliyoituma kwenye mtandao wa kijamii wa X kuwa: Tukio hilo liliripotiwa Jumatatu katika gereza kubwa zaidi la taifa la Makala katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kinshasa.
Lukoo amebainisha kuwa: "Idadi ya muda ya waliopoteza maisha ni 129, ikiwa ni pamoja na 24 waliouawa kwa kupigwa risasi baada ya kupuuza onyo."
Waziri huyo wa DRC ameongeza kuwa, wafungwa wengine waliaga dunia kutokana na mkanyagano au kukosa hewa, na kwamba majeruhi 59 wapo mikononi mwa vyombo vya dola.
Kabla ya hapo, afisa mmoja wa gereza alisema wafungwa wote waliojaribu kutoroka jela wameuawa, na kwamba serikali imeanzisha uchunguzi wa tukio hilo.
Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa, jaribio hilo lililofeli la kutoroka jela lilitukia saa nane usiku wa kuamkia jana Jumatatu. Baadhi ya wafungwa wameliambia shirika hilo kuwa, sauti za milio ya risasi na mayowe ya wafungwa zilihinikiza ndani ya nje ya gereza hilo wakati wa tukio hilo.
Ikumbukwe kuwa, wanamgambo wenye silaha wamekuwa wakivamia magereza na jela za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuachilia huru mamia ya wafungwa.