Jeshi: Waasi 500 wa ADF tangu kuanza 'Operesheni ya Shujaa'
(last modified Sat, 19 Aug 2023 03:53:04 GMT )
Aug 19, 2023 03:53 UTC
  • Jeshi: Waasi 500 wa ADF tangu kuanza 'Operesheni ya Shujaa'

Mamia ya waasi wa kundi linalojiita Allied Democratic Forces (ADF) wameuawa tangu vikosi vya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vianzishe Operesheni ya Shujaa dhidi ya genge hilo mashariki ya Kongo.

Hayo yamesemwa na Meja Jenerali Dick Olum, Kamanda wa Operesheni Shujaa iliyoanzishwa na majeshi ya nchi hizo mbili jirani mnamo Novemba 31 mwaka 2021.

Amesema katika kipindi hicho, wanamgambo 50 wa ADF wamekamatwa wakiwa hai huku wengine 31 wakijisalimisha tangu operesheni hiyo kabamba ianze.

Meja Jenerali Dick Olum wa Uganda amesema: ADF karibu itaingia katika daftari la historia. Tumepunguza uwezo wao wa kuanzisha vita, tumekandamiza nguvu kazi yao na kuharibu silaha zao. Ari yao hivi sasa ipo chini tangu operesheni ianze, na tumekuwa tukiwafuatiliwa katika maeneo ya Tokomeka, Ituri, Kyabi, Boga na Zuguruka.

Hii ni katika hali ambayo, watu 55 wameripotiwa kuuawa na waasi hao wa ADF na waitifaki wao mashariki mwa DRC kuanzia Julai 31 hadi Agosti 14. Katika eneo la Batangi-Mbau mjini Beni, watu 19 waliuawa ndani ya usiku mmoja katika kipindi hicho.

Wapiganaji wa ADF

ADF ni moja ya makumi ya makundi yenye silaha yanayoeneza vurugu mashariki mwa Kongo, mengi yakiwa ni urithi wa vita vya kikanda vilivyopiganwa baada ya kuanguka kwa dikteta wa muda mrefu wa taifa hilo la Afrika, Mobutu Sese Seko katika miaka ya 1990.

Hata hivyo kwa ujumla mashambulizi katika maeneo hayo yamepungua kwa kiasi kukubwa, hasa katika maeneo ambayo vikosi vya pamoja vya DRC na Uganda vimekita kambi.

 

Tags