Aug 23, 2023 10:21 UTC
  • RSF yadai kwamba imeua wanajeshi 260 wa Sudan

Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) vimedai kuwa vimewaua mamia ya askari wa vikosi vya Jeshi la Sudan, huku mapigano baina ya pande mbili hizo yakishtadi.

Taarifa iliyotolewa na RSF inasema, vikosi hivyo mbali na kuua wanajeshi 260 wa Sudan, lakini pia vimewakamata mamia ya wanajeshi wa Kikosi cha Vifaru cha jeshi hilo la serikali katika kitongoji cha Al Shagara, kusini mwa mji mkuu Khartoum.

Hata hivyo Jeshi la Ulinzi la Sudan limekanusha madai hayo ya kuuawa askari wake, likisisitiza kuwa lilifanikiwa kuzima shambulizi hilo la Jumatatu la vikosi vya RSF.

Mashuhuda wanasema makabiliano makali yanaendelea kushuhudiwa baina ya pande mbili hizo hasa mjini Khartoum, huku vikosi hasimu vikishambuliana kwa risasi, mabomu, maroketi na ndege zisizo na rubani (droni).

Mapigano ya utumiaji silaha nchini Sudan yalianza Aprili 15 kati ya vikosi vya jeshi la nchi hiyo vinavyoongozwa na Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) vinavyoongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo.

Wanajeshi wa RFS

Licha ya vita na mapigano nchini Sudan kutimiza miezi mitano sasa na kusababisha vifo vya maelfu ya watu, juhudi za upatanishi wa kimataifa za kukomesha vita hivyo na kuzileta pande zinazozozana kwenye meza ya mazungumzo bado hazijazaa matunda.

Hadi sasa usitishaji vita umetangazwa mara kadhaa nchini Sudan kwa upatanishi wa jamii ya kimataifa hususan kupitia juhudi za Saudi Arabia na Marekani, lakini pande zinazozozana zimeendelea kukiuka makubaliano hayo, na kwa sababu hiyo mapigano ya hapa na pale yanaendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Tags