Kanali Mikombe wa jeshi la DRC ahukumiwa kunyongwa
(last modified Wed, 04 Oct 2023 03:09:31 GMT )
Oct 04, 2023 03:09 UTC
  • Kanali Mikombe wa jeshi la DRC ahukumiwa kunyongwa

Kanali Mike Mikombe, kamanda wa zamani wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amehukumiwa kifo kutokana na nafasi yake kwenye mauaji ya makumi ya raia waliokuwa wakiandamana dhidi ya vikosi vya Umoja wa Mataifa.

Kanali Mikombe anatuhumiwa kutoa amri ya kuuawa waandamanaji wakati wa maandamano hayo yaliyofanyika mwezi Agosti mwaka huu 2023.

Mawakili wa afisa huyo wa zamani wa ngazi ya juu wa jeshi la Kongo DR wamesema watakata rufaa dhidi ya uamuzi huo uliotolewa na Mahakama ya Kijeshi ya nchi hiyo ya katikati mwa Afrika.

Serikali ya DRC ilitangaza kuwa, watu 43 waliuawa wakati wanajeshi walipovunja maandamano ya raia dhidi ya askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa (MUNUSCO) katika mji wa mashariki wa Goma.

Hata hivyo shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) lilisema idadi ya waandamanaji waliouawa ni zaidi ya 50, mbali na 56 kujeruhiwa na zaidi ya 150 kukamatwa.

Kanali Mikombe

Taarifa iliyotolewa na Human Rights Watch (HRW) wiki chache baada ya mauaji hayo ilisema, maafisa "walioamuru matumizi ya nguvu zisizo halali wanapaswa kusimamishwa kazi, kuchunguzwa, na kuwajibika katika kesi za haki na za umma".

Itakumbukwa kuwa, maandamano mengine ya kupinga uwepo wa vikosi vya MONUSCO katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yaliyofanyika Julai 2022 yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 15, wakiwemo askari 3 wa kulinda amani huko Goma na katika mji wa Butembo.

Tags