Moise Katumbi kugombea urais Kongo DR mwezi Disemba
(last modified Thu, 05 Oct 2023 03:16:52 GMT )
Oct 05, 2023 03:16 UTC
  • Moise Katumbi kugombea urais Kongo DR mwezi Disemba

Millionea na mwanasiasa wa upinzani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Moise Katumbi amewasilisha jina lake kwa ajili ya kugombea urais nchini humo.

Gavana huyo wa zamani wa eneo lenye utajiri wa madini la Katanga anatazamiwa kuchuana na Rais Félix Tshisekedi anayewania muhula wa pili wa urais katika uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Chama chake kilitangaza habari hiyo jana Jumatano. Msemaji wa chama hicho, Cherubin Okende aliuawa katika mazingira ya kutatanisha mwezi Julai mwaka huu.

Katumbi kupitia taarifa yake amesema, chama chake katika wiki zijazo kitatangaza mipango yake ya kurejesha usalama, kumaliza vita, kubuni nafasi za ajira na kuimarisha huduma za jamii iwapo kitashinda uchaguzi huo.

Katumbi (58) alizuiwa kurejea nyumbani kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2018. Hata hivyo aliruhusiwa kurejea nyumbani mwaka 2019, na kisha kufutiwa tuhuma za kufadhili uharamia.

Rais Tshisekedi (kulia) na Martin Fayulu

Muungano wa Sacred Union for the Nation (USN) tayari umeshamteua Rais Félix Tshisekedi kuwa mgombea wa uchaguzi wa urais wa Disemba 2023 kwa tiketi ya muungano huo.

Aidha kiongozi mwandamizi wa upinzani nchini humo, Martin Fayulu, ametangaza kwamba atagombea uraia katika uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Disemba 20. Mgombea mwingine mashuhuri wa urais ni daktari wa Congo ambaye alishinda Tuzo ya Amani ya Nobel kwa kazi yake ya kutibu waathirika wa ubakaji, Dakta Denis Mukwege. 

Tags