Maelfu ya Watunisia waandamana kuwaunga mkono Wapalestina
Maelfu ya wananchi wa Tunisia wamefanya maandamano wakionyesha mshikamano wao na wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina sanjari na kulaani jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina.
Walioshiriki katika maandamano hayo ya jana Alkhamisi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tunis ni wanachama wa makundi ya kiraia, wawakilishi wa mashirika ya kutetea haki za binadamu, wanaharakati wa kisiasa, mawakili, na wanafunzi wa shule za sekondari.
Waandamanaji hao wanaopinga jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza wamekosoa uamuzi wa baadhi ya madola kuisaidia na kuanzisha uhusiano wa kawaida na serikali ya kifashisti ya Benjamin Netanyahu, ambayo inaendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya raia wasio na hatia wa Gaza.
Juzi pia, wananchi wa Afrika Kusini walifanya maandamano wakionyesha mshikamano wao na watu wanaodhulumiwa wa Palestina na kutangaza uungaji mkono wao kwa mapambano ya ukombozi wa Palestina
Maandamano hayo ya wananchi wa Tunisia na Waafrika Kusini ni sehemu ndogo ya maandamano yanayoendelea katika pembe mbalimbali za dunia kuunga mkono mapambano ya kupigania ukombozi wa Palestina na kupinga jinai na mauaji yanayoendelea kufanywa na utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais Kais Saied wa Tunisia alikanusha vikali madai kuwa taifa hilo lina azma ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel. Alisema kadhia ya Palestina ina umuhimu mkubwa kwa taifa hilo, na kusisitiza kwamba kuna haja ya milki za Palestina kurejeshwa kwa wananchi wa Palestina.
Wananchi wa Tunisia wamekuwa wakilaani dhulma na mauaji ya wananchi madhulumu wa Palestina yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel kila leo. Hivi karibuni, Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia ililaani hujuma za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza na kuitaka jamii ya kimataifa kutekeleza majukumu yake mkabala wa Palestina.