ICJ yaanza kusikiliza hatua za kibinadamu zinazopaswa kutekelezwa na Israel
Mwanadiplomasia wa Palestina jana Jumatatu aliiambia Mahakama ya Kilele ya Umoja wa Mataifa kwamba Israel inawaua, inawafurusha raia wa Kipalestina na kuwashambulia wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu huko Gaza.
Ammar Hijazi, mwanadiplomasia wa Palestina nchini Uholanzi ameiambia Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) mjini Hague kwamba utawala wa Israel unakiuka sheria za kimataifa katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan. Amesema, Israel inawasababishia njaa, kuua na kuwafukuza raia wa Kipalestina katika makazi yao na kuzishambulia taasisi za misaada ya kibinadamu ambazo zinafanya jitihada za kunusuru maisha ya raia.
Kikao cha jana cha mahakama ya ICJ mjini Hague Uholanzi kilichunguza ombi lililowasilishwa mwaka jana na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambalo liliitaka mahakama hiyo kupima wajibu wa kisheria wa utawala wa Israel baada ya utawala huo kulizuia Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada kwa Ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA kuendesha shughuli zake.
Mahakama ya ICJ imeendesha kikao chake huku mfumo wa misaada ya kibinadamu wa Ukanda wa Gaza ukikaribia kusambaratika. Utawala wa Kizayuni wa Israel umezuia kuingizwa Gaza misaada ya chakula, mafuta ya petroli, dawa za matibabu na suhula nyingine za kibinadamu tangu tarehe pili mwezi Machi mwaka huu.
Aidha Israel ilianzisha tena mashambulizi dhidi ya watu wa Gaza Machi 18 mwaka huu, na hivyo kukiuka mapatano ya usitishaji mapigano ikisema kuwa lengo lake ni kushinikiza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas kuwaachilia mateka zaidi wa utawala huo.