Kesi ya kwanza ya Zika yaripotiwa Guinea-Bissau
Serikali ya Guinea-Bissau imebuni kamati ya dharura ya afya baada ya kuripotiwa kesi tatu za kwanza za kirusi hatari cha Zika.
Taarifa ya Wizara ya Afrika ya nchi hiyo imesema kuwa, kesi za ugonjwa huo hatari zimeripotiwa katika eneo la Bijagos na kwamba serikali imebuni kamati maalumu inayoongozwa na Waziri Mkuu Baciro Dja ili kuzuia kusambaa kwa kirusi hicho, wakati huu ambapo nchi hiyo ndogo ya magharibi mwa Afrika inajikusanya baada ya kukumbwa na ugonjwa wa Ebola.
Kirusi hatari cha Zika kiliripotiwa kuibuka barani Afrika kwa mara ya kwanza katika Visiwa vya Cape Verde magharibi mwa bara hilo mwezi uliopita. Mkrugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) barani Afrika, Matshidisho Moeti alisema, kesi hiyo ya Cape Verde ni ushahidi kuwa kirusi cha Zika sasa kimesambaa hadi nje ya bara la Amerika na kuingia Afrika.
Kirusi cha Zika kuligunduliwa kwa mara ya kwanza barani Afrika mwaka 1947 na hakikuhesabiwa kuwa hatari hadi kilipoibuka upya mwaka jana nchini Brazil na kusababisha wanawake walioambukizwa kuzaa watoto wenye ubongo mdogo.