Kampeni za uchaguzi wa rais zang'oa nanga Kongo DR
(last modified Sun, 19 Nov 2023 13:46:21 GMT )
Nov 19, 2023 13:46 UTC
  • Kampeni za uchaguzi wa rais zang'oa nanga Kongo DR

Makumi ya maelfu ya wagombea wa viti mbalimbali wakiwemo wagombea 26 wa kiti cha rais katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamezindua rasmi kampeni za uchaguzi huo leo Jumapili.

Kampeni hizo zinatazamiwa kuendelea kwa muda wa mwezi mmoja. Uchaguzi mkuu ukiwemo wa rais katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umepangwa kufanyika tarehe 20 ya mwezi ujao wa Disemba.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo CENI, watu milioni 44 kati ya idadi jumla ya Wakongomani milioni 100, wamesajiliwa na kutimiza masharti ya kushiriki zoezi hilo la kidemokrasia la Disemba 20.

Kwa ujumla, kuna wagombea zaidi ya 25,00 watakaowania Ubunge, 44,000 watakaogombea tawala za mikoa na wengine zaidi ya 31,000 watakauchuana kwenye uongozi wa mabaraza ya manispaa. 

Mapema mwezi huu, wagombea kadhaa wa upinzani katika uchaguzi wa rais DRC walisema kuwa, kuna haja ya kuweko mazungumzo kabla ya kufanyika uchaguzi mwezi ujao, ili kujadili masuala muhimu.

Heka heka za uchaguzi uliopita DRC

Wagombea hao Moïse Katumbi, Martin Fayulu, Dakta Denis Mukwege, Franck Diongo, Josée-Marie Ifoku na Seth Kikuni wana wasiwasi kuhusu kutokuwepo kwa uwazi katika mchakato wa ufadhili wa uchaguzi.

Rais Felix Tshisekedi anatarajiwa kutetea kiti chake huku awamu yake yake kwanza ya uongozi ikikabiliwa na ukosoaji mkubwa.

Utawala wa Rais Tshisekedi umekumbwa na hali ngumu ya uchumi, janga la Covid-19, mripuko wa Ebola, ukosefu wa usalama hasa mashariki ya nchi ambako wapiganaji wa kundi la M23 waliteka sehemu ya maeneo ya mashariki na kusababisha kuvunjika kwa uhusiano wa nchi hiyo na Rwanda.

Tags