UN inajiandaa kuanza kuwaondoa taratibu wanajeshi wake huko Kongo
(last modified Tue, 19 Dec 2023 08:03:59 GMT )
Dec 19, 2023 08:03 UTC
  • UN inajiandaa kuanza kuwaondoa taratibu wanajeshi wake huko Kongo

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo Jumanne linatarajiwa kukubali ombi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo la kuondolewa nchini humo askari wa kulinda amani wa umoja huo (MONUSCO).

Kikosi cha askari jeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) kitaondoka nchini humo licha ya kuwepo wasiwasi kuhusu hali ya machafuko mashariki mwa nchi hiyo.  

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kesho Jumatano itaendesha uchaguzi wa Rais na Bunge; siku ambayo inakwenda sambamba na kumalizika muda wa kuhudumu askari jeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo (MONUSCO). Maeneo ya mashariki mwa Kongo yamekuwa yakiathiriwa na ukosefu wa amani na mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi ya wanamgambo wenye silaha. 

Wanamgambo wanaobeba silaha Kongo 

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa miezi kadhaa sasa imekuwa ikitoa wito wa kuharakishwa kuondoka kikosi cha (MONUSCO) nchini humo yaani kuanzia mwishoni mwa mwaka huu wa 2023 badala ya mwishoni mwa mwaka kesho licha ya hali tete ya ndani.  

Serikali ya Kinshasa inaamini kuwa kikosi cha (MONUSCO) kimeshindwa kuwalinda raia mkabala wa mashambulizi ya makundi ya wanamgambo wenye silaha mashariki mwa Kongo kwa miongo mitatu sasa.  

Tuhuma hizi za Kongo zinafanana na zile zilizotolewa na nchi nyingine za Kiafrika khususan serikali ya Mali ambayo pia imetaka kuondoka haraka nchini humo askari jeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa (MINUSMA).

 

Tags