Dec 22, 2023 07:56 UTC
  • Ufaransa kufunga ubalozi wake nchini Niger

Wanadiplomasia wa Ufaransa wameeleza kuwa nchi hiyo imechukua uamuzi wa kufunga ubalozi wake huko Niamey mji mkuu wa Niger.

Ufaransa imechukua uamuzi huu wa nadra kushuhudiwa baada ya hatua iliyochukuliwa na Niger tarehe 12 mwezi huu ya kutangaza kuwa wanajeshi wote wa Ufaransa wanatakiwa kuwa wameondoka nchini humo kufikia leo Ijumaa tarehe 22 Disemba. 

Wanajeshi wa Ufaransa huko Niger 

Hitilafu zilipamba moto katika uhusiano wa Ufaransa na Niger baada ya jeshi kuchukue mamlaka ya katika mapinduzi yaliyojiri Niger Julai 26 mwaka huu.

Katika nchi kama Burkina Faso na Mali pia tawala za kijeshi zilizotwaa madaraka baada ya mapinduzi zililirejesha nyuma jeshi la Ufaransa lakini wanadiplomasia wa nchi hiyo wameendelea kuhudumu katika nchi hizo; hata hivyo Ufaransa inasema kuwa huko Niger hali imekuwa tofauti. Serikali ya Ufaransa mwishoni mwa Septemba mwaka huu ilichukua uamuzi wa kuwaondoa wafanyakazi wengi wa ubalozi wake mjini Niamey baada ya shambulio la Julai 30 katika ubalozi huo na kuzingirwa na wanajeshi wa Niger.  

Wanadiplomasia hao wa Ufaransa wanadai ubalozi wa nchi hiyo huko Niger hauwezi kutekeleza majukumu yake ya kawaida, na kwamba kwa kuzingatia hali hiyo wameamua kuufunga haraka iwezekanavyo. Wamesema kwa muktadha huo wanapaswa kuwaachisha kazi wafanyakazi wazawa na kuwalipa fidia kulingana na sheria za nchi.

Tags