Dec 25, 2023 02:42 UTC
  • Makumi ya magaidi wa al Shabaab waangamizwa Somalia

Wizara ya Ulinzi ya Somalia imetangaza kuwa makumi ya magaidi wa kundi la wanamgambo wa al Shabaab wameangamizwa kusini mwa nchi hiyo.

Shirika la habari la Farsi limeripoti kuwa, Wizara ya Ulinzi ya Somalia jana Jumapili imetangaza kuwa katika siku tatu zilizopita jeshi la nchi hiyo limekomboa sehemu kubwa ya ardhi zilizokuwa zinashikiliwa na kundi la kigaidi la al Shabaab  lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida. 

Ripoti ya Wizara ya Ulinzi ya Somalia imeeleza kuwa magaidi wa al Shabaab wasiopungua 130 wameangamizwa katika mapigano kati yao na jeshi la Somalia katikati mwa majimbo ya Hir Shabelle na Jubaland kusini mwa nchi hiyo.  

Magaidi wa al Shabaab 

Katika mapigano hayo, jeshi la Somalia limenasa silaha na zana kadhaa za kivita kutoka katika maficho ya magaidi wa al Shabaab. Kundi la kigaidi la al Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida linatekeleza mashambulizi ya umwagaji damu huko Somalia tangu mwaka 2007 ili kuiondoa madarakani serikali ya nchi hiyo. 

Tags