UN: Walinda amani wote wataondoka Kongo DR mwishoni mwa 2024
(last modified Sun, 14 Jan 2024 07:40:16 GMT )
Jan 14, 2024 07:40 UTC
  • UN: Walinda amani wote wataondoka Kongo DR mwishoni mwa 2024

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambacho kimesaidia katika vita dhidi ya waasi kwa zaidi ya miongo miwili sasa, kitaondoka kikamilifu nchini humo ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.

Bintou Keita, Mkuu wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  MONUSCO alisema jana katika mkutano na vyombo vya habari huko Kinshasa mji mkuu wa nchi hiyo kuwa bila shaka Monusco itaondoka Kongo kabla ya kumalizika mwaka huu wa 2024 baada ya kuhudumu nchini humo kwa miaka 25.

Tangazo hilo limetolewa baada ya serikali ya Kongo kukitaka kikosi hicho cha kudumisha amani cha   Umoja wa Mataifa kuondoka nchini, ikisema imeshindwa kuwalinda raia dhidi ya makundi ya wanamgambowenye silaha.

Makundi mengi yenye silaha, ikiwa ni pamoja na Allied Democratic Forces (ADF) na M23, yamejizatiti mashariki mwa Kongo khususan katika maeneo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na majimbo ya Ituri, ambapo raia wanakabiliwa na ukosefu wa amani na kulazimika kuyahama makazi yao.

Awamu ya kwanza askari jeshi wasiopungua 2,000 wa Umoja wa Mataifa wataondoka huko Kivu Kusini hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu na hivyo  idadi  ya wanajeshi wa MONUSCO watakaokuwa wamesalia huko Kongo itakuwa 11,500.

Kikosi cha MONUSCO kitaondoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika awamu tatu; ambapo kambi 14 za kijeshi zilizoko Kivu kusini zitachukuliwa na vikosi vya usalama vya Kongo, amesema Bintou Keita.

 

Tags