Misri yalalamikia hatua ya Italia ya kukata ushirikiano wake na Cairo
Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imeelezea kusikitishwa kwake na hatua ya Italia ya kusimamisha ushirikiano wake na Cairo.
Shirika la habari la Rusia al Yaum limeripoti habari hiyo leo Alkhamisi na kunukuu taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri ikielezea kusikitishwa na uamuzi wa bunge la Italia wa kupasisha muswada wa Baraza la Sanate la nchini hiyo wa kusimamisha kuipatia Misri vipuri vya ndege za kivita.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imesema, hatua hiyo ya Italia inakinzana na malengo ya pamoja na nchi hizo mbili ya kupambana na ugaidi, kwani uamuzi huo wa Rome utakuwa na taathira mbaya katika juhudi za Misri wa kukabiliana na ugaidi.
Itakumbukwa kuwa, tarehe 25 Januari 2016 mwanafunzi wa chuo kikuu raia wa Italia mwenye umri wa miaka 28 anayejulikana kwa jina la Giulio Regeni alitoweka nchini Misri na tarehe 3 Februari mwili wake ukaokotwa pembeni mwa barabara.
Mashirika ya haki za binadamu yamesema kuwa, mwili wa kijana huyo ulikuwa na majeraha ya mateso, jambo ambalo linaonesha kuwa vikosi vya usalama vya Misri ndivyo vilivyomuua.
Jambo hilo limeikasirisha Italia na kuamua kusimamisha ushirikiano wake na serikali ya Misri.