Jan 28, 2024 13:34 UTC
  • Umoja wa Afrika wapongeza amri ya ICJ ya kutaka kuzuiwa mauaji ya kimbari Gaza

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amekaribisha na kupongeza uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) wa kuitaka Israel ichukue hatua zote zinazohitajika kuzuia vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Katika taarifa, Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema: AU inakaribisha maagizo ya muda na ya dharura yaliyotolewa na ICJ katika shauri lililowasilishwa na Afrika Kusini. 

Amesema uamuzi uliotolewa Ijumaa na mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi umesisitizia haja ya kuheshimiwa sheria za kimataifa na kuitaka Israel ifungamane na majukumu yake chini ya Hati ya Mauaji ya Kimbari.

Kadhalika afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Afrika amesema anatumai kwamba Israel itachukua hatua za kutekeleza amri hiyo ya Mahakama ya Kimataifa ya ICJ na isitishe vita katika Ukanda wa Gaza kwa misingi ya ubinadamu.

Mwenyekiti wa Tume ya AU amebainisha kuwa, Wapalestina wasio na hatia ndio wanaolipa gharama kubwa na kupitia machungu, mateso na mauaji kwenye mgogoro huo wa Gaza.

Majaji wa Mahakama ya ICJ

Halikadhalika Moussa Faki Mahamat ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, na hasa mataifa makubwa yenye nguvu duniani, kubeba jukumu la kusitisha mgogoro huo.

Mataifa mbali mbali duniani kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Qatar, Misri, Saudi Arabia na Jordan yamepongeza uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwa shauri la mashtaka ya Afrika Kusini dhidi ya Israel, unaoiamuru Israel iache vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina na kuchukua hatua za kuwasaidia raia.

Tags