Feb 12, 2024 04:37 UTC
  • Wananchi wa Ghana washerehekea kurejeshwa turathi zilizoibiwa na Marekani

Wananchi wa Ghana wanaendelea kusherehekea hatua ya kurejeshwa nchini humo turathi za thamani zilizokuwa zimeibiwa zaidi ya karne moja na nusu iliyopita na askari wa mkoloni Muingereza na kuhifadhiwa Marekani.

Shirika la habari la Africa News liliripoti habari hiyo jana Jumapili na kueleza kuwa, turathi hizo muhimu za kihistoria za Ghana zilizokuwa Marekani zilirejeshwa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi mnamo Februari 8, baada ya kupita zaidi ya miaka 150.

Sehemu ya turathi hizo zilizoibiwa na vikosi vya Uingereza na kuhifadhiwa kwenye jumba moja la makumbusho nchini Marekani ni taji la Kifalme la 'Asante' na vinyago vya thamani ambavyo sasa vimerejeshwa katika sehemu yake ya asili- Kasri ya Manhyia.

Wananchi wa Ghana wamesema kurejeshwa turathi hizo za thamani kutasaidia katika mchakato wa kupoza majeraha ya nafsi yaliyosababishwa na wakoloni; na kukuza utalii wa nchi hiyo.

Wakoloni mbali na kumwaga damu za Waafrika, lakini pia walipora rasilimali za bara hilo

Waghana wanatazamia turathi zaidi zilizobiwa na Wamagharibi enzi za ukoloni zitarejeshwa nchini humo katika miezi ijayo, ambapo aghalabu ya bidhaa hizo za thamani zitarejeshewa Ufalme wa Ashanti. 

Kurejeshwa sehemu ya turathi hizo za thamani za Ghana kumefungua tena mjadala mkubwa wa kidiplomasia kuhusu dafina na vitu vya kale vya thamani vilivyoporwa na wakoloni barani Afrika.

Nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikitaka kurejeshwa turathi na dafina zao za kale zilizoporwa na wakoloni wa Ulaya wakati wa kipindi cha ukoloni.  Weledi wa mambo wanatumai kuwa, maelfu ya turathi za kihistoria zilizoibiwa wa wakoloni barani Afrika katika enzi za ukoloni zitarejeshwa katika nchi zao za asili.

Tags