Mwakilishi wa Afrika Kusini ICJ: Israel imefanya mauaji ya kimbari Gaza
Mwakilishi wa Afrika Kusini katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ametangaza kuwa, uvamizi na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza yanatisha zaidi kuliko mfumo wa ubaguzi wa rangi, apartheid.
Mwakilishi wa Afrika Kusini katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki alisema jana Jumanne katika kikao cha pili kinachojadili kadhia ya uvamizi wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina kwamba, ukatili na mashambulizi ya utawala wa Israel Ukanda wa Gaza ni kinyume cha sheria za kimataifa.
Mwakilishi huyo wa Afrika Kusini ametilia mkazo udharura wa kuhukumiwa Israel na kuongeza kuwa: Wapalestina wa Ukanda wa Gaza wanaishi katika eneo la mbali na lililokatwa vipande vipande na kuzungukwa na wanajeshi wa Kizayuni; na uvamizi wa Israel katika eneo hilo umewanyima haki yao ya kuishi.
Afrika Kusini imesisitiza ulazima wa kuhukumiwa utawala unaofanya mauaji ya kimbari wa Israel na kusema: Hatua za utawala wa Kizayuni zitaifanya hali kuwa mbaya zaidi kwa Wapalestina, watu wa Palestina wanapaswa kujiamulia hatima yao wenyewe, na jamii ya kimataifa inapaswa kuunda mifumo ya kuwalinda na kuheshimu haki yao ya kuamua hatima yao wenyewe.
Kwa upande wake, Ziyad Bin Maashi Al-Attiyah, mwakilishi wa Saudi Arabia katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki amesema kuwa Israel haina nia ya kufanya mazungumzo na lengo lake ni kufanya mauaji ya kimbari na kuwatimua watu wa Palestina kwa lazima katika ardhi yao.
Al-Attiyah ameongeza kuwa, licha ya kulaaniwa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki na Baraza la Usalama, Israel inaendelea kutekeleza sera zake za ujenzi wa vitongoji vya walowezi katika ardhi ya Palestina.
Ahmed Laaraba, mwakilishi wa Algeria katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki pia amesisitiza kuwa hatua za Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza zinaonyesha ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, na sera zake zina matokeo mabaya ya kisheria ambayo yanaziathiri nchi zote na Umoja wa Mataifa.