Feb 24, 2024 10:44 UTC
  • Rais wa Sudan Kusini achukua hatua kukomesha mapigano mashariki mwa DRC

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir siku ya Alhamisi alizitembelea Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), katika nafasi yake kama mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), katika jaribio la kuzuia mvutano unaoongezeka kati ya majirani hao watatu.

Kituo cha kwanza cha safari ya Rais Kiir kilikuwa Kigali katika juhudi za kupunguza mzozo Mashariki mwa DRC ambao umeshika kasi tangu kuondoka kwa Vikosi vya Kikanda vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF), ambavyo muda wake wa kuhudumu ulimalizika mwishoni mwa mwaka jana.

Katibu Mkuu wa EAC Dk Peter Mathuki akiwa Kigali alisema kuwa Rais wa Rwanda Paul Kagame na Kiir walitoa wito wa kuungwa mkono na mchakato wa Nairobi unaoongozwa na EAC na mchakato wa Luanda.

Mchakato wa Luanda, unaoongozwa na Rais wa Angola Joan Lorenco, unalenga kutuliza mvutano kati ya Rwanda na DRC, nchi ambazo zinalaumiana kuhusu uungaji mkono waasi, wakati Mchakato wa Nairobi ni msukumo wa mazungumzo unaoongozwa na rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta katika kujaribu kutuliza pande zinazozozana ndani ya DRC kwa kuwaleta mezani mahasimu wote ikiwa ni pamoja na kuwahimiza waasi kuweka silaha chini.

Kiir pia alikutana na Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, ambaye ameilaumu Rwanda kwa kuunga mkono waasi wanaoipinga serikali yake. Aidha Rais Kiir amekutana na Rais wa DRC Felix Tshisekedi, katika juhudi za kutafuta mwafaka wa kurekebisha mvutano kati ya nchi hizo tatu wanachama wa EAC. Serikali ya DRC inasisitiza kuwa Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23 ambao wamekuwa wakitekeleza mauaji mashariki mwa DRC. Hatahivyo serikali ya Rwanda imekanusha madai yote mawili ya Burundi na DRC.

Tangu kujiondoa kwa EACRF mwezi Disemba mwaka jana, mapigano kati ya jeshi la DRC (FARDC) na waasi wa M23 yameshika kasi katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Aidha, DRC ilikataa kuongoza muda wa kuhudumu kikosi cha Afrika Mashariki bada ya Tshisekedi kukosoa kikosi hicho kwa kushindwa kutekeleza dhamira yao ya kuwaondoa waasi wa M23 na makundi mengine yenye silaha ambayo yalikataa kujisalimisha.

Tangu kuondolewa kwa EACRF nchini DRC, Tshisekedi amegeukia Jumuiya ya Maendeleo ya Afrika Kusini (SADC) ambayo tangu wakati huo imetuma vikosi vyake kupambana na waasi wa M23.