Umoja wa Mataifa watiwa wasiwasi na mapigano yanayoendelea Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i10897-umoja_wa_mataifa_watiwa_wasiwasi_na_mapigano_yanayoendelea_sudan_kusini
Mapigano yaliyoshtadi katika siku kadhaa zilizopita huko Sudan Kusini yamemfanya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kueleza wasiwasi wake kutokana na machafuko yanayoendelea huko Juba mji mkuu wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 09, 2016 11:31 UTC
  •  Umoja wa Mataifa watiwa wasiwasi na mapigano yanayoendelea Sudan Kusini

Mapigano yaliyoshtadi katika siku kadhaa zilizopita huko Sudan Kusini yamemfanya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kueleza wasiwasi wake kutokana na machafuko yanayoendelea huko Juba mji mkuu wa nchi hiyo.

Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa jana Ijumaa alitoa taarifa akitangaza kuwa kuendelea ghasia na mapigano ya silaha huko Juba kati ya vikosi vya askari watiifu kwa Rais Salva Kiir na wale wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini Riek Machar kunaonyesha namna pande zilizotia saini makubaliano ya amani ya nchi hiyo zinavyopinga mchakato huo. Katika taarifa hiyo Ban Ki-moon amezitaka pande zinazozozana huko Sudan Kusini kuheshimu makubaliano ya amani ya nchi hiyo.

Ripoti zinasema kuwa pande mbili za wapinzani wa serikali ya Sudan Kusini na vikosi vya jeshi la nchi hiyo zimepigana kwa siku kadhaa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Juba.

Lul Ruai Koang, Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini ametangaza kuwa wanajeshi wawili wanaomuunga mkono Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini wameuawa katika mapigano yaliyojiri Alhamisi usiku katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba na wanajeshi wengine wawili wamejeruhiwa. Afisa huyo wa jeshi la Sudan Kusini amevituhumu askari watiifu kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa nchi hiyo, Riekk Machar kuwa ndio walioanza kukifyatulia risasi kituo kimoja cha upekuzi cha vikosi vya serikali. Siku kadhaa zilizopita pia mapigano yaliongezeka katika maeneo mengine ya Sudan Kusini mbali na yale yaliyoukumba mji mkuu wa nchi hiyo Juba.

Mivutano ya ndani ilianza huko Sudan Kusini mwezi Disemba mwaka 2013 kufuatia kujitokeza hitilafu kati ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo na Makamu wake Riek Machar. Hata hivyo pande husika katika mgogoro wa nchi hiyo mwezi Agosti mwaka jana zilisaini makubaliano ya amani ili kuhitimisha vita vya ndani baada ya hali ya mambo kuwa mbaya na kufuatia upatanishi wa baadhi ya nchi. Hata kama mapigano yangali yanaendelea huko Sudan licha ya kutiwa saini makubaliano ya amani, lakini hatimaye pande husika katika mzozo wa nchi hiyo zilitangaza kuanza kushirikiana ili kufanikisha utekelezaji wa mchakato wa makubaliano hayo; na kwa msingi huo, Riek Machar kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini mwezi Aprili mwaka huu alirejea katika mji wa Juba na akachaguliwa kuwa Makamu wa Rais baada ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa akiwa pamoja na Rais Salva Kiir wa nchi hiyo.

Wachambuzi wengi wa mambo na taasisi za kimataifa walitarajia kuwa mgogoro wa ndani uliodumu kwa miaka kadhaa sasa huko Sudan Kusini ungemalizika baada ya kusainiwa makubaliano ya amani. Hata hivyo wapo waliotabiri kuwa mchakato wa kutekeleza makubaliano hayo utakabiliwa na matatizo na vizuizi mbalimbali kwa kuzingatia hitilafu kubwa zlizopo kati ya pande husika.

Weledi hao wanasema kuwa mchakato wa kutekeleza makubaliano ya amani ya Sudan Kusini hadi kufikia sasa umekuwa wa mwendo wa kinyonga; na jambo hilo mdilo limeufanya mgogoro wa nchi hiyo kuwa mkubwa zaidi. Mapigano yangali yanaendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo kati ya wafuasi wa Riek Machar na Salva Kiir na kila upande unautuhumu mwingine kuwa chanzo cha kuendelea mapigano hayo.

Kutapakaa silaha mikononi mwa makundi mbalimbali huko Sudan Kusini ni moja ya sababu za kuendelea mapigano na machafuko nchini humo. Weledi wa mambo wanasema pia kwamba nchi za Magharibi na utawala wa Kizayuni zingali zinaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Nchi hizo zinaendelea kutuma shehena za silaha haramu kwa makundi yanayozoana huko Sudan Kusini.

Ukweli wa mambo ni kuwa, kuendelea hali ya mchafukoge na mapigano nchini Sudan Kusini kunaziandalia fursa baadhi ya nchi za Magharibi na utawala haramu wa Kizayuni wa kupora maliasili za nchi hiyo. Hayo yote yanafanyika katika mazingira ambayo hali ya raia wa Sudan Kusini pia inaipotowa kuwa ni mbaya. Ripoti za taasisi mbalimbali za kimataifa zinaonyesha kuwa, wakazi wengi wa Sudan Kusini wanahitaji msaada wa haraka wa chakula na dawa.

Katika mazingira hayo, Rais wa Sudan Kusini na Makamu wake wanapasa kuchukua hatua za kivitendo ili kutekeleza makubaliano ya amani na wakati huo huo kuwatolea wito wa amani na utulivu wafuasi wao ili kusitisha mapigano nchini. Pande mbili hizo pia zinapasa kufanya juhudi za kukusanya silaha haramu na hivyo kuhitimisha machafuko na vita vya miaka kadhaa huko Sudan Kusini.