Wakuu wa majeshi ya SADC wakutana Goma kujadili M23
(last modified Sun, 03 Mar 2024 07:40:29 GMT )
Mar 03, 2024 07:40 UTC
  • Wakuu wa majeshi ya SADC wakutana Goma kujadili M23

Majenerali na maafisa waandamizi wa majeshi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wamekutana mjini Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kujadili stratajia ya kuimarisha operesheni dhidi ya waasi wa M23.

Msemaji wa Jeshi la DRC, Jenerali Sylvain Ekenge amenukuliwa na shirika la habari la Iran Press akisema kuwa, mkutano huo wa majenerali wa nchi za DRC, Afrika Kusini, Burundi, Malawi na Tanzania umejikita katika suala la kubuni stratajia ya kuimarisha operesheni za kijeshi za kuzima harakati za kundi la waasi wa M23.

Mmoja wa wakazi wa Goma, Passy Mubalama ameiambia Iran Press kuwa, kuna haja ya kutumia njia zisizo za mabavu na fujo kuhitimisha vita na mapigano mashariki ya Kongo DR.

Mkutano wa majenerali na maafisa waandamizi wa majeshi ya nchi wanachama wa SADC umefanyika katika hali ambayo, tayari jumuiya hiyo ya kikanda imeanza kuchangia askari wake waliotumwa huko DRC katika vita dhidi ya waasi wa M23.

Habari zaidi zinasema kuwa, Afrika Kusini, Malawi na Tanzania ndizo nchi za jumuiya ya SADC ambazo zimeanza kupeleka wanajeshi wao huko DRC.

Image Caption

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ilialika kikosi hicho cha SADC baada ya kusema kuwa haijaridhika na wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC ambao walitakiwa kupambana na waasi wa M23.

Kongo DR imekuwa ikimtuhumu jirani yake Rwanda kuwa inaliunga mkono kundi la waasi wa M23, madai ambayo yamekanushwa na Kigali, lakini yanaungwa mkono na Marekani, Ufaransa, Ubelgiji na wataalamu wa Umoja wa Mataifa.

Tags