Mali yasema ECOWAS haikuisaidia kupambana na ugaidi
Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) haijafanya lolote kuzisaidia nchi za Sahel kupambana na ugaidi, amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali Abdoulaye Diop.
Waziri Diop ameeleza sababu za nchi yake kujiondoa katika shirika hilo wakati wa majadiliano kwenye Kongamano la 3 la Kidiplomasia la Antalya nchini Uturuki siku ya Jumapili.
Akifafanua nukta hiyo amesema:"Tukichukua mfano wa ECOWAS na mpango wake wa kupambana na ugaidi, hatukuona chochote, hakuna msaada. Walituacha kutatua tatizo wenyewe. Kwa hiyo hatukuona umuhimu wa kukaa katika shirika hilo."
Aidha alifichua kuwa, baadhi ya washirika ambao walitaka kufanya kazi na nchi za Sahel ndio walikuwa chanzo cha kuenea kwa ugaidi na kuufadhili.
Waziri Diop amebaini kuwa, Mali, Niger na Burkina Faso zimetangaza kuchukua hatua za kuimarisha usalama wao ndani kwa kuunda Muungano wa Nchi za Sahel (AES).
Aidha aliongeza kuwa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Mali baada ya mapinduzi havikwa vya haki. Idadi ya wahanga wa ugaidi nchini Mali, Burkina Faso na Niger iliongezeka mara tano baada ya 2016, na watu 4,000 waliuawa na magaidi na watu wenye itikadi kali katika nchi hizi mwaka 2019.
Niger, Mali na Burkina Faso ni nchi tatu zenye umuhimu mkubwa katika eneo la Magharibi mwa Afrika ambazo katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni zimeshuhudia matukio makubwa ya kisiasa kwa kadiri kwamba na hivi sasa nchi hizo zinatawaliwa na serikali zilizo dhidi ya ukoloni wa Ufaransa na madola ya kibeberu.
Viongozi wa kijeshi wa nchi hizo wanaungwa mkono na wananchi kutokana na kufanikiwa kwao kuwatimua askari wa madola ya kibeberu ya Magharibi kama vile Ufaransa kwenye nchi hizo.
Kwa hakika nchi hizo tatu za Niger, Mali na Burkina Faso ambazo zina rasilimali nyingi katika eneo la Afrika Magharibi, zimekuwa zikipewa umuhimu maalumu na nchi za kikoloni, haswa Ufaransa, na katika miaka ya hivi karibuni jeshi la Ufaransa liliimarisha kuwepo kwake kijeshi katika nchi hizo kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.
Hata hivyo, hali ya eneo hilo kama vile kuongezeka harakati za kigaidi na kuenea kwake barani Afrika, kulidhihirisha zaidi uzembe na kutoheshimu nchi hizo ahadi zao za kuboresha amani na usalama na kusaidia kuondoa athari za ukoloni barani humo.