Mar 05, 2024 07:40 UTC
  • Mohamed Badie
    Mohamed Badie

Mahakama ya Misri imemhukumu kifo kiongozi wa chama cha Ikwanul Muslimin (Muslim Brotherhood), Mohamed Badie, na viongozi wengine saba wa harakati hiyo baada ya kuwatia hatiani kwa eti kupanga vitendo vya ukatili kwa "madhumuni ya kigaidi" wakati wa mgomo wa Cairo mwaka 2013.

Upande wa Mashtaka ya Umma uliwatuhumu watu hao kuwa, Julai 2013 "waliongoza kundi lililolenga kupindua utawala kwa nguvu na kushambulia watu binafsi na vituo vya jeshi, polisi na vituo vya umma, na kutumia ugaidi kwa ajili ya kufikia malengo yao.”

Wakati huo, kundi la Ikhwanul Muslimin lilipanga mgomo wa kuketi katika Uwanja wa Rabaa al-Adawiya mjini Cairo kupinga kitendo cha jeshi kumpindua Rais aliyekuwa amechaguliwa na wananchi kwa njia za kidemokrasia, Mohamed Morsi, Julai 2013.

Mwezi Agosti mwaka huo huo, vikosi vya usalama vya Misri vilitawanya kwa nguvu mgomo huo, suala ambalo lilisababisha mauaji ya zaidi ya watu elfu moja, wakiwemo makada na wafuasi wa Muslim Brotherhood.

Mohamed Badie

Baadaye serikali ya Misri ilianzisha msako mkali dhidi ya viongozi na wafuasi wa harakati hiyo kubwa na kongwe zaidi la kisiasa nchini humo na kuwakamata maelfu ya wanachama wake ambao wengi wamehukumuwa vifungo vya jela.

Viongozi kadhaa wa harakati hiyo ya Ikwanul Muslimin pia wamehukumiwa kifo. 

Mnamo Novemba 2013, chama hicho kiliwekwa rasmi katika orodha ya "makundi ya kigaidi" nchini Misri.

Tags