Mar 17, 2024 02:11 UTC
  • UN yazitaka pande za Sudan kuweka chini silaha, kuwalinda raia wakati wa Ramadhani

Umoja wa Mataifa umezitaka pande zinazozozana Sudan kuweka chini silaha na kuwalinda raia wakati huu wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Anayehusika na Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura amesema kuwa Sudan inasumbuliwa na mwaka mzima wa vita na kusisitiza kuwa mapigano yanaendelea Sudan licha ya Baraza la Usalama kupitisha azimio la kusimamishwa vita katika mwezi huu wa Ramadhani. 

"Huu ni wakati wa kupatikana suluhu; pande hasimu zinapasa kusitisha mapigano, kuwalinda raia na kutoa mwanya wa kufikishwa misaada ya kibinadamu kwa wathiriwa", amesema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Anayehusika na Masuala ya Kibinadamu. 

Sudan imetumbukia katika mapigano kati ya jeshi la nchi hiyo linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kinachoongozwa na Kamanda Hamdan Dagalo. 

Burhan na Dagalo 

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa watu wasiopungua 13,900 wameuawa na wengine zaidi ya milioni nane wamelazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi tangu kuanza vita huko Sudan mwezi Aprili mwaka jana. 

Makubaliano kadhaa ya kusitisha mapigano Sudan yameshindwa kusitisha vita nchini humo. 

Tags