Mapigano mapya yaripotiwa baina ya jeshi la Sudan na RSF huko Darfur
Wimbi jipya la mapigano limeripotiwa kuanza baina ya wanajeshi wa Sudan na wapiganaji wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka RSF katika jimbo la Darfur, magharibi mwa nchi hiyo.
Wanaharakati wa kundi la kiraia la Al-Fasher wameliambia shirika la habari la Anadolu kuwa, mapigano hayo yalianza jana Ijumaa na yanaendelea mpaka sasa.
Habari zaidi zinasema kuwa, watu kadhaa wamejeruhiwa baada ya nyumba zao kushambuliwa kwa maroketi karibu na mji wa Al-Fasher, makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini.
Inaelezwa kuwa, silaha nzito nzito zimetumika katika wimbi hilo jipya la makabiliano jimboni Darfur. Hata hivyo, mpaka tunamaliza kuandaa taarifa hii, hakuna taarifa iliyokuwa imetolewa na jeshi la Sudan au RSF kuhusiana na vita hivyo.
Wimbi la jipya la mapigano limeanza Sudan katika hali ambayo, Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch hivi karibuni lilisema kuwa, mfululizo wa mashambulizi ya vikosi vya wanamgambo vya Sudan katika eneo la Darfur unaongeza uwezekano wa "mauaji ya halaiki".
Aidha raia katika mji huo na eneo pana la Darfur tayari wanasumbuliwa na kiwango kikubwa cha njaa, lakini uwasilishaji wa msaada wa chakula umekuwa wa kusuasua kutokana na vikwazo vya ukiritimba na mapigano yanayoendelea katika maeneo hayo.
Mapigano ya silaha yalianza huko Sudan Aprili 15 mwaka jana kati ya jeshi la nchi hiyo (SAF) linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan ambaye ni kiongozi wa Sudan na wanamgambo wa RSF ambao kamanda wao ni Hamdan Dagalo.
Hadi sasa juhudi za upatanishi wa kimataifa za kuhitimisha mapigano hayo ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 13,000 na takriban milioni 8.5 kulazimika kuwa wakimbizi ndani ya nje ya Sudan, zimegonga mwamba.