Rais wa Nigeria aliagiza jeshi liwasake walioua askari 16 Delta
Rais wa Nigeria Bola Ahmed Tinubu ameliamrisha jeshi la nchi hiyo kuwasaka na kuwafikisha katika vyombo vya dola wahusika wa mauaji ya wanajeshi 16 wa nchi hiyo katika jimbo la kusini la Delta.
Rais Tinubu pia amelaani vikali shambulio hilo lililopelekea kuuawa wanajeshi 16 wa nchi hiyo wakiwemo mameja wawili na kapteni mmoja na kusisitiza kuwa, hujuma hiyo ni shambulio la moja kwa moja dhidi ya taifa.
"Waliotekeleza jinai hii ya kioga na kihaini lazima watawajibishwa na kuadhibiwa,"ameeleza Rais wa Nigeria ambaye aliahidi kukabiliana na changamoto za usalama nchini humo tangu aingie madarakani.
Amesema: Nimetoa ridhaa na mamlaka kamili kwa makao makuu ya Wizara ya Ulinzi na mkuu wa majeshi, ili kuhakikisha kuwa askari waliouawa na raia ambao ni wahanga wa shambulio hilo wanapata haki.
Rais wa Nigeria amesema uchunguzi unaoendelea umepelekea kutiwa mbaroni watu kadhaa wanaohusishwa na shambulio hilo la Jumamosi iliyopita katika jimbo la kusini la Delta.
Wanajeshi waliouawa katika hujuma hiyo walikuwa wametumwa katika eneo hilo la kusini mwa Nigeria kwenda kudhibiti mapigano baina ya jamii za Okuama na Okoloba.
Msemaji wa Jeshi la Nigeria, Brigedia Jenerali Tukur Gusau amesema operesheni kabambe ya kuwasaka wahalifu waliofanya mauaji hayo huko Delta inaendelea, na kwamba hadi sasa wamefanikwa kutwaa silaha na zana za kijeshi zilizokuwa zinatumiwa na wanajeshi waliouawa ili zikiishie kwenye mikono ya wanamgambo na waasi.