Mar 22, 2024 02:33 UTC
  • Spika wa Bunge Ghana amkosoa Rais kwa kutopasisha sheria dhidi ya LGBT

Spika wa Bunge la Ghana, Alban Bagbin amemjia juu Rais Nana Akufo-Addo wa nchi hiyo kwa kutoidhinisha kuwa sheria muswada wa kupambana na ushoga na ubaradhuli LGBTQ+ takriban mwezi mmoja baada ya kupasishwa kwake na Bunge.

Bagbin amesema hatua ya Rais Akufo-Addo kuuweka pembeni muswada huo 'kwa muda' ni kinyume cha sheria na kutishia kuwa, Bunge la nchi hiyo halitaidhinisha majina ya mawaziri wapya walioteuliwa na kiongozi huyo wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Ofisi ya Rais Akufo-Addo imesema muswada huo haujapasishwa kuwa sheria kwa kuwa wanasubiri uamuzi wa mahakama. Mahakama moja ya nchi hiyo hivi karibuni ilipokea mafaili mawili ya kupinga muswada huo.

Spika wa Bunge la Ghana amesema kutopasishwa kwa muswada huo kunaenda kinyume na Katiba ya nchi, mbali na kuibua mkwamo na msuguano baina ya mhimili wa Bunge na Ofisi ya Rais. 

Bunge la Ghana mwishoni mwa mwezi uliopita wa Februari, lilipitisha muswada huo wa kupambana ufuska wa ushoga, ubaradhuli na usagaji, baada ya takriban miaka mitatu ya majadiliano.

Bunge la Ghana

Muswada huo mpya umeainisha kifungo cha hadi miaka mitatu jela kwa yeyote atakayepatikana na hatia ya kujitambulisha kama LGBTQ+ au kujihusisha ya maingiliano ya kingono ya watu wenye jinsia moja. Vilevile unaweka kifungo cha juu zaidi cha miaka mitano jela kwa kuunda au kufadhili vikundi vya mashoga.

Bunge la Ghana lilipasisha muswada huo yapata miezi miwili baada ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis kutoa idhini rasmi kwa makasisi kubariki ndoa za watu wa jinsia moja katika kanisa hilo. Uamuzi huo wa Papa umezua hasira kubwa na kupingwa hata na makanisa Katoliki katika maeneo mbalimbali ya dunia hususan barani Afrika. 

Tags