Rais wa Colombia aendeleza kampeni ya kumkosoa Rais Trump wa Marekani
Katika siku za hivi karibuni, Rais Gustavo Petro wa Colombia, ameendeleza ukosoaji mkali dhidi ya Rais Donald Trump wa Marekani na sera za utawala wake.
Akizungumza na waandishi wa habari, Petro amesema, "Trump hastahili chochote isipokuwa jela, kwa kushiriki katika mauaji ya kimbari. Hakuna uharamu wowote kuhusu kutumia matokeo ya Mkataba wa Roma, iwe nchini Marekani au popote pengine," ameongeza Rais Petro. "Ikiwa Trump ataendelea kuhusika katika mauaji ya halaiki, kama anavyofanya mpaka leo hii, hastahili chochote ila jela, na jeshi lake halipaswi kumtii," amesema Rais wa Colombia na kuongeza kuwa, "Marekani na Israel sio sehemu ya Mkataba wa Roma wa ICC, lakini Colombia ni mwanachama."
Petro pia alipofika New York kuhudhuria kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa alijiunga na waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina nje ya makao makuu ya umoja huo. Akiwa hapo alitoa hotuba kali na kutaka kuundwa kwa jeshi la kimataifa kwa ajili ya kuwaokoa Wapalestina. Aliwahimiza wanajeshi wa Marekani waanzishe uasi na “wasielekeze bunduki kwa raia wala wasitii amri za Trump, bali watii sauti ya ubinadamu.” Awali, katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Petro alihimiza mataifa ya ukanda wa Kusini wa dunia kuunda kikosi cha kijeshi cha kimataifa kwa ajili ya kupambana na dhulma inayoungwa mkono na Marekani na NATO, kauli zilizowapelekea wajumbe wa Marekani kuondoka ukumbini.
Baada ya kushiriki maandamano jijini New York, Marekani ilitangaza kufuta visa ya Petro. Rais huyo alipuuzilia mbali hatua hiyo, akiitaja kuwa ishara ya dharau ya Washington kwa sheria za kimataifa. Wizara ya Mambo ya Nje ya Colombia pia ililaani hatua hiyo, ikisema inakiuka misingi ya Umoja wa Mataifa, na kutoa wito wa kuchaguliwa kwa nchi mwenyeji isiyoegemea upande wowote kwa taasisi hiyo ya kimataifa.
Katika kipindi cha urais wa Gustavo Petro, uhusiano kati ya Colombia na Marekani umekumbwa na misukosuko, hasa kutokana na tofauti za kimtazamo kuhusu sera za ndani, za kikanda na za kimataifa. Kwa muhtasari, tofauti hizo zinaweza kufafanuliwa kama ifuatavyo:
1.Vita vya Gaza na Msimamo wa Kuunga Mkono Palestina
Rais Petro amelaani vikali hatua za Israel huko Gaza, akizitaja kama “mauaji ya kimbari.” Msimamo wake dhidi ya sera za Marekani katika eneo la Asia Magharibi umechochea mvutano wa kidiplomasia na kufutwa kwa visa yake.
2. Kusitisha Ununuzi wa Silaha kutoka Marekani
Rais Petro, akijibu uingiliaji wa Washington, ametangaza kuwa Colombia haitanunua tena silaha kutoka Marekani, na badala yake itatafuta vyanzo mbadala vya zana za kijeshi.

3. Ukosoaji wa Sera za Kupambana na Dawa za Kulevya
Rais Petro amezitaja sera za jadi za kupambana na mihadarati kuwa zimefeli, akisisitiza haja ya mbinu zenye utu zaidi. Ameeleza kuwa serikali yake imekamata kiasi kikubwa cha kokaini kuliko serikali zilizotangulia.
4. Kukaribiana na Serikali ya Venezuela
Wakati Marekani ina uhasama na Venezuela chini ya urais wa Nicolas Maduro, Rais Petro ameonyesha nia ya kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Venezuela.
5. Migongano kuhusu Mazingira na Nishati
Rais Petro anasisitiza umuhimu wa kuachana na uchumi unaotegemea mafuta na kuwekeza katika nishati mbadala—msimamo unaopingana na maslahi ya makampuni ya petroli Marekani.
6. Mgogoro wa Uhamiaji na Changamoto katika Umoja wa Mataifa
Rais Petro amekataa kupokea raia waliotimuliwa na Marekani, akiituhumu Washington kwa kudhalilisha demokrasia na kushambulia mamlaka ya kitaifa. Ameitaka dunia kuunda kikosi cha amani kwa ajili ya kuzuia mauaji ya kimbari yanayoendelezwa na utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza kwa uungaji mkono wa Marekani.
Mivutano hii inaashiria mabadiliko ya msimamo wa Colombia kutoka kuwa mshirika wa jadi wa Marekani hadi kuwa mkosoaji wa sera za Washington katika ngazi ya kikanda na kimataifa.