Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i11041-kikao_cha_baraza_la_usalama_la_umoja_wa_mataifa_kuhusu_sudan_kusini
Wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wametoa taarifa wakitaka kuhitimishwa mapigano katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 11, 2016 08:28 UTC
  • Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Sudan Kusini

Wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wametoa taarifa wakitaka kuhitimishwa mapigano katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba.

Taarifa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imewataka majirani wa Sudan Kusini kutoa ushirikiano unaotakiwa kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi kwa njia za amani mgogoro wa sasa wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Kikosi cha kimataifa cha kusimamia amani kilichotumwa Sudan Kusini na wanachama wa Umoja wa Mataifa na ambacho kinajulikana kwa jina la UNMISS kingali katika nchi hiyo.

Pamoja na hayo wasimamia amani hao hawajaweza kuzuia kuibuka duru mpya ya mapigano katika mji wa Juba.

Nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimewataka wanasiasa wa pande mbili huko Sudan Kusini kuvidhibiti vikosi vyao ili kuzuia kuenea mapigano hayo katika maeneo mengine ya nchi hiyo. Mapigano mapya nchini Sudan Kusini yaliibuka sambamba na maadhimisho ya mwaka wa tano tangu nchi hiyo ipate uhuru.

Mapigano hayo yalitokea katika mji mkuu Juba baina ya wanajeshi watiifu kwa Rais Salva Kiir na wale wanaomuunga mkono kiongozi wa zamani wa waasi Riek Machar ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais kwa mujibu wa makubaliano ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Riek Machar alirejea Aprili mwaka huu huko Juba na kukubali kuchukua jukumu la Makamu wa Rais katika serikali ya Umoja wa kitaifa. Mapigano kati ya pande mbili ni ya kwanza kutokea tangu kuundwa serikali hiyo.

Sudan Kusini ilijitenga rasmi na Sudan Julai 9 mwaka 2011 na kuwa nchi mpya barani Afrika.

Baada ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa huko Sudan Kusini kulijitokeza matumani katika duru za Kiafrika juu ya kurejea amani na uthabiti katika nchi hiyo na chuki na adawa kuzikwa katika kaburi la sahau.

Hata hivyo matumaini hayo yameyeyuka kwani tangu wakati huo hadi leo, hali ya usalama na kisiasa katika nchi hiyo haijabadilika.

Machafuko na vitendo vya utumiaji mabavu vinaendelea na kila siku iendayo kwa Mungu kunashuhudiwa idadi zaidi ya raia wa nchi hiyo wanaokuwa wahanga wa machafuko.

Ripoti zinaonesha kuwa, katika machafuko ya hivi karibuni huko Sudan Kusini watu wenye silaha wamekuwa wakiwalenga pia raia na hata askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa. Herve Ladsous, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini ameitathmini hali ya sasa ya Sudan Kusini na kusema kuwa inatia wasiwasi.

Serikali ya Kenya kwa upande wake sambamba na kuonesha wasiwasi wake wa kuendelea mapigano mjini Juba imesema kuwa, kupoteza maisha watu 272 waliokuwa wakitaka kuishi maisha bora na ya ufanisi ni jambo la kusikitisha mno.

Takwimu za Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR zinaonesha kuwa, takribani watu milioni mbili na laki sita wa Sudan Kusini ni wakimbizi huku akthari yao wakiwa ni watoto. Sehemu nyingine ya taarifa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imewaonya viongozi wa Sudan Kusini kwamba, nchi hiyo itawekewa vikwazo vya silaha na kiuchumi.

Aidha wajumbe wa baraza hilo wameitaka jamii ya kimataifa kuonyesha radiamali chanya mkabala na matukio ya Sudan Kusini.