Apr 29, 2024 02:36 UTC
  • Burkina Faso yakanusha ripoti ya HRW, yasema haina mashiko

Serikali ya Burkina Faso imekanusha vikali na kulaani tuhuma ilizosema hazina msingi zilizotolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch ambalo limelituhumu jeshi la serikali ya nchi hiyo kuwa lilihusika na mauaji ya mwezi Februari mwaka huu 2024 katika vijiji vya Nodin na Soro kaskazini mwa nchi hiyo.

Waziri wa Mawasiliano wa Burkina Faso, Rimtalba Jean Emmanuel Ouedraogo ameeleza kuwa mauaji yaliyojiri katika vijiji vya Nodin na Soro yalipelekea kufunguliwa uchunguzi wa kisheria na kwamba wakati wakisubiri kukamilika uchunguzi huo na kubainika ukweli juu wa wahusika, Human Rights Watch kwa mtazamo wake limeamua kutangaza matokeo ya uchunguzi huo. 

Itakumbukwa kuwa shirika la HRW liliyataja mauaji hayo ya umati kuwa miongoni mwa uhalifu mbaya zaidi kuwahi kufanywa na jeshi la Burkina Faso tangu mwaka 2015. 

Shirika la HRW lenye makao yake mjini New York, Marekani limeeleza kuwa mauaji hayo ya umati yaliyofanywa katika vijiji viwili huko Burkina Faso yanaonekana kuwa ni sehemu ya kampeni ya kijeshi dhidi ya raia wanaotuhumiwa kushirikiana na makundi yenye silaha, na yanaweza kutambuliwa kuwa ni jinai dhidi ya binadamu.

Serikali ya Burkina Faso imesema kuwa, kampeni inayoenezwa na vyombo vya habari kuhusu tuhuma dhidi ya serikali ya nchi hiyo inaonyesha kikamilifu nia mbaya yenye lengo la kushusha hadi ya jeshi la Burkina Faso.  

Image Caption

Alhamisi iliyopita Jeshi la Burkina Faso lilituhumiwa na HRW kuwa limewauwa kiholela raia 223, wakiwemo watoto wengine wengi, katika mashambulizi dhidi ya vijiji viwili vinavyotuhumiwa kushirikiana na waasi wenye silaha. 

Tags