Apr 29, 2024 11:31 UTC
  • Haniyah: Netanyahu na baraza lake la kigaidi wanapaswa kukamatwa

Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, amelaani vikali jinai za kutisha za utawala haramu wa Israel huko Gaza, akitaka Waziri Mkuu wa utawala huo na baraza lake la mawaziri wa kigaidi wafikishwe mbele ya mahakama za kimataifa ya kushughulikia jinai za kivita.

Ismail Haniyah alikuwa akizungumza katika mkutano wa Jumapili na mjukuu wa Nelson Mandela, Nkosi Zwelivelile Mandela, katika mji wa bandari wa Uturuki wa Istanbul.

Katika kikao hicho Haniyah amelaani vikali jinai za kutisha zinazofanywa na utawala ghasibu wa Israel katika vita vyake vya mauaji ya halaiki dhidi ya Ukanda wa Gaza unaozingirwa.

Amesisitiza wajibu wa jumuiya ya kimataifa kuhusiana na matukio yanayoendelea Gaza, akisisitiza kwamba ikiwa haki itatolewa, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na wajumbe wake wa baraza la mawaziri la kigaidi lazima wakamatwe kwa vitendo vyao vya uhalifu.

Haniyah pia amepongeza hatua ya kihistoria ya Afrika Kusini ya kuwasilisha kesi ya kisheria dhidi ya utawala ghasibu wa Israel kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ikiishutumu Israel kwa kufanya mauaji ya kimbari huko Gaza.

Kwingineko katika matamshi yake, Haniyah amewashukuru watu na serikali ya Afrika Kusini kwa uungaji mkono wao usio na kikomo kwa kadhia ya Palestina.

Amesema msimamo uliochukuliwa na hayati kiongozi wa nchi hiyo, Nelson Mandela, kuhusu suala la Palestina ulikuwa na mwelekeo wa kweli wa kibinadamu na kimaadili, na unapingana kabisa na uungwaji mkono wa kipofu na wa upendeleo unaotolewa kwa Israel na Marekani na nchi nyingine za Magharibi.

Mandla Mandela, kwa upande wake, amempa Haniyeh salamu zake za rambirambi kufuatia kuuawa shahidi kwa watoto na wajukuu wake.

Amesisitiza tena uungaji mkono wa nchi yake kwa kadhia ya Palestina hadi kuasisiwa taifa huru la Palestina huku mji wake mkuu ukiwa ni ule unaokaliwa kwa mabavu wa al-Quds.