Apr 30, 2024 07:22 UTC
  • Arab League: Lengo la Utawala wa Kizayuni ni kuifuta Palestina pamoja na haki zake

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amesema, lengo la vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Ghaza ni kufuta uwepo wa Palestina na haki zake na vilevile kulifuta moja kwa moja suala la Palestina.

Ahmad Abul Ghaith, ameongeza kuwa, suala la Palestina liko kwenye hali na marhala ya kufa na kupona katika muktadha wa kukabiliana na vita angamizi vinavyoendeshwa na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza na Palestina na kwa ajili ya kukabiliana na jinai ya mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo dhidi ya Wapalestina hususan katika Ukanda wa Gaza, yanayoendelea kwa takribani miezi saba sasa. 
 
Tangu tarehe 7 Oktoba 2023, utawala ghasibu wa Kizayuni ulianzisha mauaji makubwa ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza dhidi ya watu wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina kwa uungaji mkono kamili wa nchi za Magharibi.
Marekani ndiye kinara wa uungaji mkono kwa Israel katika vita na mauaji ya kimbari unayofanya Ghaza

Kimya cha jamii ya kimataifa na taasisi za haki za binadamu kwa jinai za utawala ghasibu wa Israel, kimesababisha kuendelea kuuawa wanawake na watoto wa Kipalestina katika vita vya kinyama vilivyoanzishwa na utawala huo haramu.

 
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi katika katika eneo hilo kutokana na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni tangu Oktoba 7, 2023 hadi sasa imefikia watu elfu 34,488 na idadi ya waliojeruhiwa imefikia elfu 77,643.../

 

 

Tags