Ofisi ya Haki za Binadamu ya UN yabainisha wasiwasi wake kuhusu kukandamizwa wahamiaji Tunisia
Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa jana ilibainisha wasiwasi wake kuhusu "kuongezeka ukandamizaji na vitendo vya mabavu dhidi ya wahamiaji nchini Tunisia. Ofisi hiyo imesema kuwa haki za wahamiaji wote zinapasa kulindwa.
Ravina Shamdasani Msejai wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa amewaambia waandishi wa habari huko Geneva kwamba wana wasiwasi kuhusu kuongezeka vitendo vya mabavu na ukandamizaji wanaofanyiwa wahamiaji huko Tunisia aghalabu yao kutoka kusini mwa jangwa la Sahara, watu binafsi na taasisi zinazofanya kazi kuwasaidia raia hao.
Shamdasani pia amesema kuwa wakati huo huo wanashuhudia ongezeko la matumizi ya maneno ya udhalilishaji na ubaguzi wa rangi dhidi ya wahamiaji weusi na Watunisia weusi," Ameeleza kuwa ofisi ya haki za binadamu imerekodi matukio ya kukamatwa kiholela na kuwekwa kizuizini watetezi wa haki za binadamu, wanasheria na waandishi wa habari wanaoikosoa serikali ya Tunisia pamoja na sera zake za uhamiaji.
Ameongeza kuwa, hujuma ya uvamizi ulioripotiwa wiki iliyopita katika ofisi ya Chama cha Wanasheria wa Tunisia unadhoofisha utawala wa sheria na kukiuka viwango vya kimataifa kuhusu ulinzi wa uhuru na kazi ya mawakili,
Volker Turk Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu amezihimiza mamlaka za serikali kuheshimu na kulinda uhuru wa kujieleza, uhuru wa kufanya mikutano na kukusanyika kwa amani kama ilivyotiliwa mkazo katika Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa ambao Tunisia imeusaini.