Jun 08, 2024 04:08 UTC
  • Rais wa Afrika Kusini: ANC itaunda serikali ya umoja wa kitaifa

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ametangaza kuwa chama tawala cha African National Congress (ANC) kimekubali kuunda serikali ya umoja wa kitaifa baada ya kupoteza wingi wa kura katika uchaguzi wa wiki iliyopita.

"Tumekubaliana kuvikaribisha vyama vya siasa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, chaguo bora zaidi la kuipeleka nchi yetu mbele," ameeleza Ramaphosa mbele ya waandishi wa habari baada ya kuhitimisha mkutano wa siku moja wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho.
 
Amesema, taratibu za serikali hiyo ya umoja wa kitaifa itakayoundwa na ANC zitazingatia hali iliyopo kwa sasa nchini.
 
Ramaphosa amefafanua zaidi kwa kusema: "madhumuni ya serikali ya umoja wa kitaifa lazima, kwanza kabisa, yawe ni kukabiliana na masuala muhimu ambayo Waafrika Kusini wanataka yashughulikiwe. Masuala haya ni pamoja na uzalishaji wa ajira na ukuaji wa uchumi wetu utakaokuwa jumuishi na gharama kubwa za maisha”.
 
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, serikali ya umoja wa kitaifa itaangalia utoaji wa huduma, uhalifu na rushwa, yote ambayo yalikuwa masuala kuu ya uchaguzi yaliyoibuliwa na vyama vya siasa.

Chama cha ANC, ambacho kiliwahi kuongozwa na mwanasiasa wa kimataifa Nelson Mandela, kilitawala siasa za Afrika Kusini kwa miongo mitatu iliyopita hadi kilipopoteza wingi wake katika uchaguzi wa taifa na wa majimbo tarehe 29 Mei.

 
Chama hicho, ambacho kilikuwa kikipata zaidi ya 60% katika chaguzi zote tangu 1994, isipokuwa 2019, wakati ushindi wake ulipopungua hadi 57.5%, kilipata 40.18% tu ya kura katika uchaguzi wa mwaka huu. Hali hiyo imekiweka chama hicho katika wakati mgumu kuweza kuunda serikali peke yake.
 
Ramaphosa amekiri pia kuwa chama chake kimetambua kwamba watu wa Afrika Kusini walibainisha matakwa yao wakati wa uchaguzi wa wiki iliyopita na wao wanayakubali matokeo.
 
Amefafanua zaidi kwa kusema: "sasa tunasema kama Kamati Kuu ya Taifa ya ANC kwamba tumesikia wasiwasi wa watu wa Afrika Kusini na tumesikia masikitiko yao na kutambua matarajio yao".
 
Rais wa Afrika Kusini ameendelea kueleza kwamba NEC ilikubali kuwa ili nchi iweze kuondokana na changamoto zinazoikabili, kunahitajika serikali ya umoja na ushirikiano kati ya vyama vya siasa.
 
"Kutokana na matokeo ya chaguzi hizi, ni wazi kuwa Waafrika Kusini wanatarajia viongozi wao kufanya kazi pamoja ili kukidhi mahitaji yao. Wanatutarajia kupata muafaka wa kutatua tofauti zetu na kuchukua hatua kwa manufaa ya kila mtu,’’ amemalizia kiongozi huyo.../

 

Tags