Jun 18, 2024 12:19 UTC
  • Serikali ya Kenya yaondoa mapendekezo ya ushuru baada ya upinzani mkali

Serikali ya Kenya Kwanza imetupilia mbali mapendekezo makuu ya ushuru ambayo yamezua taharuki miongoni mwa Wakenya katika majuma ya hivi karibuni.

Tangazo hilo limetolewa baada ya Rais William Ruto kuandaa mkutano wa kundi la wabunge katika Ikulu ya Nairobi leo.

Katika kikao na wanahabari baada ya mkutano huo, timu ya Ruto ilisema mapendekezo hayo yametupiliwa mbali kufuatia zoezi la ushirikishwaji wa umma ambalo lilishuhudia Wakenya wakiibua upinzani dhidi ya mapendekezo hayo.

Awali polisi ya Kenya iliwakamata makumi ya waandamanaji katika mitaa ya mji mkuu Nairobi huku baadhi ya Wakenya wakiandamana kupinga Mswada wa Fedha wa 2024.

Mswada wa Sheria ya Fedha nchini Kenya umezua malalamiko makubwa ya umma, huku wakosoaji wakisema kuwa utaweka mzigo wa kifedha usiofaa kwa raia ambao tayari wanakabiliana na matatizo ya kiuchumi.

 

Polisi waliokuwa wamevalia mavazi ya kawaida waliwakamata waandamanaji waliokuwa wakikusanyika katika maeneo mbalimbali ya mikutano katikati mwa jiji la Nairobi.

Kenya mojawapo ya nchi zilizoendelea kiuchumi katika Afrika Mashariki, ilirekodi mfumuko wa bei wa 5.1% kwa mwaka mwezi wa Mei, huku bei ya chakula na mafuta ikipanda kwa 6.2% na 7% mtawalia, kulingana na data za Benki Kuu. Ukuaji wa Pato la Taifa unatarajiwa kushuka hadi 5% mwaka huu, baada ya kufikia 5.6% mwaka 2023 (4.9% mwaka 2022), kulingana na utabiri wa Benki ya Dunia. Deni la umma la nchi linafikia karibu shilingi bilioni 10,000 (EUR bilioni 71), au karibu 70% ya Pato la Taifa.