Jun 20, 2024 07:03 UTC
  • WFP yapata dola milioni 37 za kusaidia wakimbizi nchini Kenya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lmetangaza kwamba limepata mchango wa dola milioni 37 za Kimarekani kama msaada wa chakula na lishe kwa wakimbizi walioko nchini Kenya, msaada ambao utaliwezesha shirika hilo kuongeza mgao kwa wakimbizi walioko hatarini zaidi katika kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakma hadi mwezi Disemba mwaka huu.

Lauren Landis, mkurugenzi wa WFP nchini Kenya amesema hayo katika taarifa yake ya jana Jumatano aliyoitoa mjini Nairobi Kenya na kuongeza kwa kusoma: "Misaada inayotolewa kwa kuzingatia viwango vya mahitaji inahakikisha kuwa watu walioko hatarini zaidi wanapewa kipaumbele kwa mujibu wa rasilimali na inapunguza idadi ya watu walioko hatarini zaidi.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa pia limesema kwamba, kwa ushirikiano na serikali ya Kenya na shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, shirika hilo limeanza kuhama kutoka kwenye hatua ya kuwapa wakimbizi msaada wa aina moja na kuja na mkakati wa kuzingatia mahitaji.

Amefafanua zaidi kwa kusema: Mkakati huo mpya utatoa msaada kwa kuzingatia usalama wa chakula na hali ya kijamii na kiuchumi ya kila familia. Kwa sasa, wakimbizi 650,000 wanaosaidiwa na WFP wanapokea kiwango sawa cha msaada wa chakula.

Moja ya kambi kubwa za wakimbizi nchini Kenya

 

Msaada huo umekuja wakati muhimu kwani kwa muda mrefu kulikuwa na upungufu wa ufadhili ambao uliilazimisha WFP kupunguza mgao wa chakula hadi rekodi ya chini ya asilimia 40.

Mbali na changamoto hizo za kifedha, hivi karibuni wakimbizi nchini Kenya wamekumbwa na athari za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na ukame na mafuriko ambayo yameharibu rasilimali zao ambazo tangu zamani zilikuwa chache.

Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, hivi sasa nchini Kenya kuna wakimbizi 775,000 kutoka nchi 20 tofauti.