Jun 21, 2024 02:45 UTC
  • Mripuko wa kipindupindu waua makumi ya watu nchini Nigeria

Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na mripuko mpya wa ugonjwa wa kipindupindu katika jimbo la Lagos, kusini magharibi mwa Nigeria imeongezeka na kufikia 21.

Kemi Ogunyemi, mshauri maalumu wa afya wa serikali ya jimbo la Lagos amesema kesi zaidi ya 400 za maradhi hayo zimeripotiwa mwezi huu pekee katika eneo hilo, huku akitoa mwito wa kufanyika jitihada za pamoja ili kuudhibiti mripuko huo.

Amesema yumkini ongezeko la vifo na kusambaa kwa kasi kwa maradhi hayo katika jiji la Lagos linalohesabiwa kuwa kitovu cha biashara cha Nigeria kumetokana na mikusanyiko mikubwa ya watu wakati wa sherehe za Idul Adh'ha iliyoadhimishwa siku chache zilizopita.

Janga hilo la kipindupindu limeendelea kuchukua roho za watu nchini Nigeria katika hali ambayo, ni asilimia 14 tu ya wananchi wa nchi hiyo yenye idadi ya watu milioni 200 ndio wenye uwezo wa kupata maji safi na salama. 

Wagonjwa wa kipindupindu hospitalin Nigeria

Maradhi ya kipindupindu yanaelezwa kuyatesa mataifa kadhaa ya Afrika Magharibi ikiwemo Nigeria, kutokana na kuongezeka idadi ya wagonjwa wa maradhi hayo.

Serikali za nchi hizo za Afrika Magharibi zinajaribu kudhibiti mripuko wa kipindupindu, ambapo afisa wa ngazi ya juu wa afya amesema kwamba, mamilioni ya watu wanapewa chanjo ili kufidia mapengo makubwa ya kinga dhidi ya ugonjwa huo huko Nigeria.

Shirika la Afya Duniani linakadiria kuwa kuna visa kati ya 1,300,000 na 4,000,000 vya kipindupindu duniani kila mwaka, na takriban watu 143,000 hufa kutokana na ugonjwa huo kila mwaka.

Tags