Mataifa yanayounda Muungano wa Sahel yanakutana leo Niamey, Niger
Viongozi wa Muungano wa Sahel wanakutana leo katika mji mkuu wa Niger, Niamey kwa ajili ya kujadilii masuala mbalimbali.
Niamey, mji mkuu wa Niger, leo ni mwenyeji wa mkutano wa kwanza wa Wakuu wa Nchi za Muungano wa Nchi za Sahel (AES), ulioundwa mwezi Septemba 2023. Kanali Assimi Goïta wa Mali na Kapteni Ibrahim Traoré wa Burkina Faso wamepokewa na mwenzao wa Niger, Jenerali Abdouramane Tiani.
Mkutano huu utafanyika kabla ya mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, uliopangwa kufanyika kesho mjini Abuja Nigeria. Nchi hizi zinazounda muunganowa Sahel zilijitoa katika jumuiya ya ECOWAS mwanzoni mwa mwaka huu.
Huu utakuwa mkutano wa kwanza wa aina yake kati ya wakuu hao watatu wa nchi, ingawa mikutano kadhaa ya nchi mbili tayari imefanyika. Wote tangu wakati huo wameipa kisogo Ufaransa, mkoloni wa zamani, na ECOWAS, ambayo wanaituhumu kuwa kibaraka wa Paris na kutowaunga mkono vya kutosha katika vita vyao dhidi ya makundi ya kigaidi.
Licha ya kujitenga huku, wakuu kadhaa wa nchi katika Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS,wanaendelea kutoa wito wa mazungumzo kati ya kambi hizo mbili. Hili ndio lengo kubwa hasa la Bassirou Diomaye Faye, rais wa Senegal ambaye, aliingia madarakani hivi karibuni, ambaye aliona kuwa maridhiano yanawezekana kati ya ECOWAS na AES.