Jul 07, 2024 11:09 UTC
  • ECOWAS: Muungano wa Sahel ni changamoto kubwa

Mkutano wa kilele wa viongozi wa Afrika Magharibi umefunguliwa leo Jumapili huku kukiwa na mizozo ya kisiasa, baada ya tawala za kijeshi katika nchi za Niger, Mali na Burkina Faso kuunda shirikisho baina yao.

Taarifa ya ECOWAS imeeleza kuwa shirikisho hilo kati ya Mali, Niger na Burkina Faso ni changamoto kuu kwa sasa kunapofanyika mkutano wa kilele wa viongozi wa Jumuiya hiyo ya Kiuchumi ya Magharibi wa Afrika; ambayo tayari inakabiliwa na matatizo mbalimbali kama ukosefu wa bajeti, uhalifu wa makundi ya wanamgambo wenye silaha n.k.   

ECOWAS: Makundi yenye silaha magharibi mwa Afrika, ni changamoto kubwa 

Nchi tatu yaani Mali, Niger na Burkina Faso zimetangaza kuunda Shirikisho jipya (AES) na kufanyika mkutano wa kwanza wa shirikisho hilo siku moja kabla ya mkutano wa viongozi wa Ecowas kumetajwa kuwa ni mtihani mwingine kwa jumuiya hiyo ya kikanda ambayo nchi hizo tatu zilijitenga nayo mapema mwaka huu. 

Itakumbukwa kuwa watawala wa kijeshi wa Mali, Niger na Burkina Faso jana Jumamosi walikutana huko Niamey, mji mkuu wa Niger ambapo walisaini mkataba unaoashiria kuundwa kwa Muungano wa Sahel na kujitoa kwao ndani ya jumuiya ya ECOWAS. 

Licha ya nchi hizo tatu kujitenga na ECOWAS, lakini wakuu kadhaa wa nchi za jumuiya hiyo ya kiuchumi wanaendelea kutoa wito wa mazungumzo kati ya kambi hizo mbili. 

Tags