Rais wa Guinea-Bissau atishia kuufukuza ujumbe wa ECOWAS
(last modified Mon, 03 Mar 2025 07:07:02 GMT )
Mar 03, 2025 07:07 UTC
  • Rais wa Guinea-Bissau atishia kuufukuza ujumbe wa ECOWAS

Rais wa Guinea-Bissau, Umaro Sissoco Embalo ametishia kuufukuza ujumbe wa kisiasa uliotumwa nchini mwake na Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS).

ECOWAS imesema katika taarifa yake jana Jumapili kwamba, ilituma ujumbe kutoka Februari 21 hadi 28 pamoja na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Afrika Magharibi na Sahel (UNOWAS) kusaidia kufikia muafaka wa jinsi ya kuendesha uchaguzi mwaka huu.

Jumuiya hiyo imefichua kuwa: "Ujumbe uliondoka Bissau mapema asubuhi ya tarehe Mosi Machi, baada ya Mheshimiwa Umaro Sissoco Embalo kutishia kuufukuza."

Mzozo kuhusu ni lini muhula wa urais wa Embalo, ulioanza mwaka wa 2020, unapaswa kumalizika umezidisha uwezekano wa kuibuka machafuko katika taifa hilo lenye historia ya mapinduzi ya kijeshi.

Upinzani wa kisiasa wa taifa hilo dogo la Afrika Magharibi unasema muda wa Embalo ulipaswa kumalizika wiki iliyopita, wakati Mahakama ya Juu ikiamua kwamba muda huo utamalizika Septemba 4. Embalo, ambaye aliongoza ECOWAS kutoka katikati ya 2022 hadi katikati ya 2023, alisema mnamo Februari 23 kwamba, uchaguzi wa rais na wabunge hautafanyika hadi Novemba 30.

Rais wa Guinea-Bissau, Umaro Sissoco Embalo

Ikumbukwe kuwa, Septemba mwaka jana, Embalo alisema kwamba hatawania muhula wa pili katika uchaguzi wa rais unaotazamiwa kufanyika Novemba. Alisema mke wake ndiye aliyemshawishi na kumtaka asigombee muhula wa pili wa urais.

Embalo alichaguliwa Januari 2020 kumrithi rais Jose Mario Vaz. Alimshinda hasimu wake Domingos Simoes Pereira aliyeibuka wa pili kwa 54% ya kura; na angeweza kugombea muhula mwingine kisheria. Rais Embalo mwenye umri wa miaka 51, hakumtaja mrithi wake.