UN: Watu milioni 4.5 wamekimbia makazi yao Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i113806-un_watu_milioni_4.5_wamekimbia_makazi_yao_ethiopia
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (UNOCHA) imetangaza kuwa, takriban watu milioni 4.5 wamekimbia makazi yao katika maeneo ya vijijini na mijini nchini Ethiopia.
(last modified 2024-07-08T00:10:39+00:00 )
Jul 08, 2024 00:10 UTC
  • UN: Watu milioni 4.5 wamekimbia makazi yao Ethiopia

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (UNOCHA) imetangaza kuwa, takriban watu milioni 4.5 wamekimbia makazi yao katika maeneo ya vijijini na mijini nchini Ethiopia.

Taarifa ya ofisi hiyo ambayo ni ya karibuni zaidi imeongeza kuwa, watu waliokimbia makazi yao ni wengi katika maeneo ya Somalia, Oromia na Tigray ya nchi hiyo ya pembe ya Afrika. 

Takwimu za UNOCHA zinaonyesha kuwa watu wengi wamekimbia makazi yao kutokana na migogoro isiyovumilika ya mwaka 2021. Takriban asilimia 56 ya wakimbizi wa ndani (IDPs) wamelazimika kuyahama makazi yao kwa zaidi ya mwaka mmoja, huku asilimia 23 wameyahama makazi yao kwa miaka miwili hadi minne.

Tathmini zinaonesha kuwa wengi wa wakimbizi hao wa ndani (IDPs), hasa wale wanaoishi katika hali ya kuhama kwa muda mrefu, wanaweza kusaidiwa kurejea maeneo yao waliyoyakimbia kutokana na vita na masaibu mengineyo. 

Tangu mwezi Januari 2022, wakimbizi wa ndani wapatao milioni 3.3 wamerejea katika maeneo yao ya asili kwenye maeneo tofauti ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Pamoja na hayo, ripoti ya ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, idadi ya wakimbizi wa ndani (IDPs) leo inafikia milioni 4.5 kutokana na uhamaji unaoendelea katika mikoa kadhaa ya Ethiopia.

Ethiopia ambayo ni nchi ya pili barani Afrika kwa kuwa na watu wengi zaidi baada ya Nigeria ina takriban watu milioni 126.5. Katika miaka ya hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia majanga mengi ikiwa ni pamoja na ghasia na machafuko ya ndani.