Misri yaandaa mkutano wa kushughulikia mzozo wa Sudan
Wajumbe wa vyama mbalimbali vya siasa vya Sudan na makundi ya kiraia wamekutana Cairo mji mkuu wa Misri kutafuta suluhu ya kisiasa ya mgogoro wa Sudan.
Wawakilishi kutoka mashirika ya kikanda na kimataifa pia wamehudhuria mkutano huo. Mkutano huo umefunguliwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Uhamiaji na Masuala ya Wageni wa Misri, Badr Abdelatty.
Katika sehemu moja ya matamshi yake, Waziri Abdelatty amesema: "Suluhu yoyote ile ya kweli ya kisiasa ya mgogoro wa Sudan lazima iwahusishe Wasudan wa kada na makundi yote na mgogoro huo utatatuliwa na Wasudan wenyewe.
Taarifa hiyo haikufafanua ni vyama au makundi gani ya Sudan yameshiriki, lakini Abdalla Hamdok, waziri mkuu wa zamani wa Sudan ambaye kwa sasa ni mkuu wa Uratibu wa Majeshi ya Kiraia na Kidemokrasia ambao ni muungano wa wananchi wa Sudan waopinga vita angamizi na atilifu vya uchu wa madaraka vinavyoendelea baina ya majenerali wa kijeshi huko Sudan ameshiriki kwenye mkutano huo.
Waziri Abdelatty amesisitiza kuwa, pande zote nchini Sudan zinapaswa kujumuishwa katika mchakato wa kutafuta amani chini ya msingi wa kuheshimiwa haki ya kujitawala ardhi yote ya Sudan pamoja na kutoingiliwa masuala ya ndani ya nchi hiyo.
Sudan imekuwa katika vita vibaya sana vya ndani tangu katikati ya mwezi Aprili 2023. Hadi tarehe 10 Mei, 2024 vita hivyo vilishasababisha vifo vya watu 16,650.
Mgogoro huo umekuwa ni mzigo mkubwa pia kwa nchi zinazopakana na Sudan, kuanzia wimbi kubwa la wakimbizi hadi uchafuzi wa mazingira.