Siku ya Kiswahili Duniani: Tuthamini lugha yetu ya Kiswahili
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i113812-siku_ya_kiswahili_duniani_tuthamini_lugha_yetu_ya_kiswahili
Maadhimisho ya siku ya Kiswahili Duniani yamefanyika katika mataifa mbalimbali huku kukitolewa miito ya kuithamini lugha hii ambayo sasa inatambuliwa na Umoja wa Mataifa.
(last modified 2024-07-08T00:40:41+00:00 )
Jul 08, 2024 00:40 UTC
  • Siku ya Kiswahili Duniani: Tuthamini lugha yetu ya Kiswahili

Maadhimisho ya siku ya Kiswahili Duniani yamefanyika katika mataifa mbalimbali huku kukitolewa miito ya kuithamini lugha hii ambayo sasa inatambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Akizungumza kwa mnasaba huo Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema “itakuwa sahihi nikisema Kiswahili ni lugha ya ukombozi, ni lugha ya umoja, ni lugha ya amani na ni lugha ya biashara.

Hivyo ametoa mwito kwa viongozi wengine duniani kukitumia Kiswahili katika kukuza mtangamano, kujenga na kulinda amani na mshikamano, kufundisha vijana na watoto elimu na maadili mema na kukuza biashara miongoni mwa nchi zao.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni akihutubia kwa njia ya video kutoka Uganda alitoa hotuba yake akirejelea maandiko ya kidini pale binadamu walipokuwa wakizungumza lugha moja wakataka kujenga mnara wa Babeli ili kufikia mbinguni.

 

Katika salamu zake za mwaka huu za siku hii Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Audrey Azoulay amezungumza mengi juu ya siku hii ikiwemo kuzungumzwa na zaidi ya watu milioni 200 duniani kote pamoja na kuwa lugha rasmi ya Muungano wa Afrika- AU na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC.

Hivi karibuni nchi Wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa zilipitisha azimio la kihistoria lililowasilishwa na Kenya na Tanzania kwa niaba ya Kundi la Afrika na kutangaza rasmi kuwa tarehe 7 Julai ni Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili.

Kiswahili ni kati ya lugha 10 zinazozungumzwa na watu wengi zaidi duniani, ikiwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 200. Ni lugha iliyoenea zaidi pia katika nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika na pia katika nchi za Asia Magharibi.