Mashahidi wa mauaji ya halaiki Shakahola kuanza kutoa ushahidi leo huko Kenya
-
Mchungaji Paul Mackenzie na wenzake
Kesi ya mauaji ya Msitu wa Shakahola inatarajiwa kuendelea kusikilizwa leo mahakamani wakati mashahidi watakapotoa ushahidi wao dhidi ya mshukiwa mkuu wa mauaji hayo, mchungaji Paul Mackenzie, na wenzake 93.
Paul Mackenzie wa Kanisa la Good News International na wenzake wanakabiliwa na makosa kadhaa yanayohusiana na ugaidi.
Miongoni mwa mashahidi wanaofikishwa mahakamani leo ni wale wanaolindwa ambao wanajua matukio ya msitu wa Shakahola yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 430 wanaoaminika kuwa waumini wa Kanisa la Good News International.
Inaaminika kuwa kanisa hilo la mchungaji Mackenzie lilitumika kama jukwaa la kupitishia itikadi kali kwa mamia ya wafuasi wake ambao baadaye waliangamia wakiwa kwenye mfungo hatari wa kujitoa uhai. Kiongozi wa Kikristo wa kanisa hilo aliwaamuru wafuasi wake wajiue kwa njaa, wao na watoto wao, ili waende mbinguni kukutana na Yesu.
Awali, mahakama iliambiwa kuwa Mackenzie alihubiri kanisani kwamba njia pekee ya kukutana na Yesu ni kujiua kwa njaa.
Mashahidi hao wanatarajiwa kufichua kilichojiri katika msitu wa Shakahola na jinsi wafuasi wa kanisa hilo walivyofundishwa itikadi kali kabla ya kukubali kufunga hadi kufa.
Mashahidi hao pia wanatarajiwa kufichua mafundisho waliyopewa, watu binafsi waliohusika na mafundisho hayo, jinsi ujumbe ulivyowasilishwa, maeneo mahususi na tarehe za shughuli hizi katika eneo la Furunzi huko Malindi kati ya 2020 na 2023.