Rais wa Nigeria ateuliwa tena kuwa mwenyekiti wa ECOWAS, ahimiza umoja
Rais Bola Tinubu wa Nigeria ametoa mwito kwa viongozi wa nchi za magharibi mwa Afrika kushikamana na kufanya kazi kwa pamoja ili kudumisha kikosi cha kikanda cha kukabiliana na matishio ya usalama yanayozidi kuongezeka katika eneo hilo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kawaida cha 65 cha Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) katika mji mkuu wa Nigeria wa Abuja, Tinubu, ambaye amechaguliwa tena kwa kauli moja kuendelea kuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo ya kiuchumi, ametilia mkazo umuhimu wa kuimarishwa kikosi cha kijeshi cha jumuiya hiyo na kuzitaka nchi wanachama kujitolea zaidi kulinda usalama na umoja wa ukanda huo.
Rais wa Nigeria amesisitiza kuwa, amani na usalama ni kitu muhimu sana kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa ECOWAS na katika kupambana na ugaidi. Amesema, mafanikio ya jumuiya hiyo hayahitaji tu nia thabiti ya kisiasa bali pia rasilimali nyingi za kifedha.
Amesema: Changamoto katika jumuiya yetu ya kiuchumi bado ni kubwa, hasa kutokana na kuenea vitendo vya kigaidi na misimamo mikali inayozidi kuenea katika ukanda wa Sahel kuelekea mataifa ya pwani.
Vilevile Rais huyo wa Nigeria amesema: "Mazingira ya kisiasa bado ni tete katika baadhi ya nchi wanachama, hasa zile zilizoshuhudia mabadiliko ya serikali kinyume na katiba."
ECOWAS hubadilisha uenyekiti wake kila mwaka. Tinubu alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo katika kikao cha 63 cha kawaida kilichofanyika mwezi Julai 2023 huko Bissau, mji mkuu wa Guinea-Bissau. Muda wa mwaka mmoja wa Tinubu ulikuwa unamalizika kesho Julai 9.