Wanajeshi wa Marekani waanza kuondoka Niger baada ya kutimuliwa, Wajerumani wanafuatia
Marekani imeanza kuondoa askari wake wote na zana zake za kijeshi huko Niger baada ya kutimuliwa kutokana na siasa zao za kibeberu. Kuondoka wanajeshi hao kumekuja kabla ya tarehe ya mwisho ya Septemba 15 waliyopewa na serikali ya Niamey ya kwamba hawatakiwi kuonekana tena kwenye ardhi ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu, wanajeshi wa Marekani wataondoka kwenye kambi ndogo mwishoni mwa wiki, huku takriban wanajeshi 500 watakaobakia wataondoka katika kambi muhimu ya ndege zisizo na rubani iliyoanzishwa Marekani ndani ya nchi hiyo mwezi Agosti.
Kambi hiyo ya droni (ndege zisizo na rubani), inayojulikana kama Nigerien Air Base 201, iko karibu na mji wa Agadez na ilijengwa kwa gharama ya dola milioni 110 za Kimarekani. Marekani ilikuwa na takriban wanajeshi 1,100 nchini Niger.
Serikali mpya ya Niger imewatimua wanajeshi wa Marekani baada ya kupinduliwa Rais wa Niger aliyekuwa kibaraka mkubwa wa nchi za Magharibi mwezi Julai mwaka jana.
Afisa mmoja wa serikali ya Niger ameliambia shirika la habari la Anadolu kwa sharti la kutotajwa jina, kwamba, lazima wanajeshi wa nchi za Magharibi wakiwemo wale wa Marekani wafukuzwe nchini Niger kwani kuweko kwao nchini humo ni tishio kwa usalama wa taifa.
Afisa mmoja wa Jeshi la Anga la Marekani aitwaye Jenerali Kenneth Ekman alisema katika mahojiano ya hivi karibuni na Shirika la Habari la Associated Press kwamba idadi ndogo ya askari wa Marekani wamehamishiwa nchi nyingine za Afrika Magharibi, lakini sehemu kubwa ya askari hao watapelekwa barani Ulaya.
Wanajeshi wa Ujerumani nao wamefukuzwa nchini Niger na wamepewa muda wa hadi Agosti 31 wahakikishe hawako tena nchini humo.