Mamia ya Wasudani wakimbia kutoka Sennar kufuatia shambulio la RSF
Vyanzo vya ndani katika mji wa Dinder, Jimbo la Sennar kusini mashariki mwa Sudan, vimeripoti leo, Jumatano - kwamba mamia ya wakazi wa eneo hilo wamehamishwa kutoka vijiji vya kaskazini mwa mji huo hadi mji wa Gedaref.
Vyanzo vya habari vimeongeza kuwa watu waliokimbia makazi yao wametumia boti za jadi kuvuka Mto Dinder kuelekea mashariki baada ya wanachama wa Rapid Support Forces (RSF) kuingia katika vijiji vya kaskazini mwa Dinder na kufyatua risasi ovyo kwenye vitongoji vya makazi ya raia na kuiba magari pamoja na kuwatesa vijana.
Ripoti zinasema kuwa wengi kati ya waliokimbia makazi yao ni watoto, wanawake na wazee ambao walielekea mashariki mwa Gedaref kwa miguu baada ya kukatika umeme, njia za mawasiliano na barabara kutokana na mvua kali.
Takwimu zinaonyesha kuwa, idadi ya watu waliolazimika kukimbia makazi yao kutoka Jimbo la Sennar inazidi 60,000, na ni zaidi ya uwezo wa mji wa Gedaref.
Mapigano ya silaha yalianza huko Sudan Aprili 15 mwaka jana kati ya jeshi la nchi hiyo (SAF) linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan ambaye ni kiongozi wa Sudan, na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) ambao kamanda wao ni Hamdan Dagalo.
Maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimishwa kuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan kutokana na vita vya kuwania madaraka kati ya majenerali wawili waitifaki wa zamani, Luteni Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan na Luteni Jenerali Hamdan Dagalo.