Jeshi la Sudan: Tumeua zaidi ya wanamgambo 100 wa RSF mjini Khartoum
(last modified Mon, 15 Jul 2024 13:15:36 GMT )
Jul 15, 2024 13:15 UTC
  • Jeshi la Sudan: Tumeua zaidi ya wanamgambo 100 wa RSF mjini Khartoum

Jeshi la Sudan (SAF) limetangaza kuwa, limeua zaidi ya wapiganaji 100 wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na kujeruhi makumi ya wengine wakati wa operesheni maalumu ya jeshi hilo katika mji mkuu Khartoum, siku ya Jumamosi pekee.

Katika taarifa yake hiyo ya jana, jeshi la Sudan limesema kuwa, vikosi tofauti vya jeshi hilo vilishirikiana katika  operesheni kadhaa kabambe katika mji mkuu Khartoum na kuua makumi ya wanamgambo wa RSF na kuharibu magari yao mengi ya kivita. 

Hayo yamekuja baada ya Gavana wa Jimbo la Khartoum, Ahmed Othman Hamza kufichua kwamba serikali imewataka wageni wanaoishi nchini Sudan kinyume cha sheria kuondoka na kurejea katika nchi zao baada ya kugundulika kuwa kuna wageni wengi wanashirikiana na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kufanya mashambulizi dhidi ya jeshi la nchi hiyo, SAF.

Gavana Ahmed ameongeza kuwa, baada ya kuanza vita, raia wa kigeni wamesambaa kwenye makazi ya watu mjini Khartoum na baadhi yao wanashirikiaina na wapiganaji wa Vikosi vya Msaada wa Haraka na hivyo ni tishio kwa usalama na utulivu wa Sudan. Amesema, uchunguzi wao unaonesha kuwa kuna makumi ya maelfu ya wageni wanaopigana bega kwa bega na RSF dhidi ya jeshi la Sudan.

Vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi nchini Sudan vilivyoanza mwezi  Aprili 2023, vimeshapelekeea zaidi ya watu 16,650 kuuawa, milioni 7.7 kuwa wakimbizi na mamia ya wengine kujeruhiwa. Hayo ni kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa mwezi uliopita na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu OCHA.