Wapinzani nchini Kenya wapinga mazungumzo ya muungano na serikali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i114210
Muungano wa upinzani nchini Kenya unaoongozwa na kiongozi wake mkongwe Raila Odinga umefutilia mbali uwezekano wa kufanya mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano na serikali kufuatia maandamano ya hivi karibuni ya kupinga nyongeza ya ushuru, maandamano ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 40.
(last modified 2024-07-18T10:44:56+00:00 )
Jul 18, 2024 10:44 UTC
  • Wapinzani nchini Kenya wapinga mazungumzo ya muungano na serikali

Muungano wa upinzani nchini Kenya unaoongozwa na kiongozi wake mkongwe Raila Odinga umefutilia mbali uwezekano wa kufanya mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano na serikali kufuatia maandamano ya hivi karibuni ya kupinga nyongeza ya ushuru, maandamano ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 40.

Haya yanajiri kufuatia mikutano iliyoanza mwaka jana kati ya serikali ya muungano wa Rais William Ruto na muungano wa Azimio wa Raila Odinga.

Maandamano yalianza Juni 18 mwaka huu yakitaka mawaziri watimuliwe kutokana na uzembe, ufisadi na kudhihirisha utajiri wao hadharani huku watu wa kawaida wakikabiliwa na mgogoro wa kupanda gharama ya maisha.

Maandamano katika mitaa ya Nairobi, Kenya

Waandamanaji walivamia bunge mnamo Juni 25, 2024 baada ya wabunge kupitisha mswada wa fedha ambao ungeongeza ushuru, ambapo polisi wamefyatua risasi na kuwaua watu wengi kwenye maandamano hayo.

Odinga kwa upande wake amenukuliwa akitaka mazungumzo yafanyike kati ya wadau tofauti wakiwemo vijana wanaoandamana ambao wanajiita Gen-Z.

Vijana hao baadaye walipuuzilia mbali wito huo wa Raila Odinga  na Rais William Ruto kuhusu kufanyika mazungumzo wakisema viongozi hao hawazingatii maslahi yao bali wanazungumza kwa niaba ya tabaka tawala.

Kundi hilo la Gen-Z  sasa linamtaka Rais William Ruto ajiuzulu na kuondoka madarakani haraka.

Wakati huo huo, polisi wa Kenya wamepiga marufuku maandamano zaidi, haswa katika wilaya ya kati ya biashara ya Nairobi wakidai kuwa makundi ya vijana wanaoandamana hawana mpangilio kwa vile hawana muundo wa kufanyiwa kazi wala kiongozi.