Aug 05, 2024 13:45 UTC
  • Takriban wahamiaji 100 wa Ethiopia waokolewa na polisi nchini Afrika Kusini

Polisi ya Afrika Kusini imeeleza kuwa imewaokoa wahamiaji 90 wa Kiethiopia waliokuwa wakishiliwa kwenye nyumba moja kinyume na ridhaa yao katika mji wa Johannesburg.

Polisi ya Afrika Kusini wamefanya msako katika nyumba moja wakimtafuta mtu aliyeripotiwa kutekwa nyaka na ndipo walipowakuta wahamiaji hao katika nyumba hiyo. Watu wawili wamekamatwa wakishukiwa kuwateka nyara watu na kushiriki katika magendo ya binadamu. Polisi ya Afrika Kusini imesema kuwa mtu huyo aliyeripotiwa kutekwa nyara, aliokolewa pia katika msako huo. 

Wahamiaji hao wa Kiethiopia wanaaminika kuuzwa kupitia magendo ya binadamu. Raia hao wa Ethiopia walikuwa wamewekwa katika vyumba vidogo ambavyo vilikuwa vimefungwa. 

Wahamiaji hao wa Kiethiopia waliookolewa huko Johannesburg Afrika Kusini wamefikishwa hospitali kwa matibabu, na watuhumiwa wawili waliotiwa mbaroni wanatazamiwa kufikishwa mahakamani hivi karibuni. 

Mwaka 2020, watu wasiopungua 64 kutoka Ethiopia walikutwa wamekufa  ndani ya kontena la mizigo huko Msumbiji. Mwaka 2022 pia, miili ya wahamiaji 30 wa Ethiopia ilipatikana katika kaburi la pamoja huko Malawi. Mwaka huo huo wa 2022 miili ya raia 27 wa Ethiopia ilikutwa imetupwa huko Zambia. 

Mamalaka mbalimbali ikiwemo Interpol zimeeleza wasiwasi wao kuhusu magendo ya wahamiaji wa Ethiopia kupitia nchi kadhaa za Afrika kuelekea Afrika Kusini. 

Tags