Aug 13, 2024 02:59 UTC
  • Mafuriko yasababisha maelfu ya watu kuhama makazi yao magharibi mwa Ethiopia

Takriban watu 16,000 wamelazimika kuhama makazi yao na kuelekea katika maeneo salama kutokana na mafuriko yaliyoathiri maeneo ya magharibi mwa Ethiopia.

Shirika la habari la Ethiopia FANA jana liliripoti kuwa wilaya nne zimeathiriwa na mvua kubwa na kusababisha mafuriko ya ghafla katika jimbo la Gambella huko Ethiopia. Mafuriko hayo yamesababisha maafa kwa nyumba na mashamba ya kilimo.

Watu walioathirika katika jimbo la Gambella wanahitaji misaada mbalimbali ili kukabiliana na athari za mafuriko na tayari wamehamishiwa katika maeneo salama. 

Gatbel Moon afisa wa kukabiliana na maafa ya kimaumbile katika jimbo hilo amesema kuwa mafuriko  kama hayo hutokea mara kwa mara katika eneo hilo, kwa kuwa mwezi Agosti unaashiria msimu wa mvua nchini Ethiopia.  Msimu huu wa mvua mara nyingi huambatana na mafuriko makubwa katika jimbo la Gambella na katika maeneo mengine ya nchi. 

Tags